WIZARA ya Afya Zanzibar kupitia Kitengo cha Maradhi yasiombukiza NCD kwa kushirikina na Serikali ya China jimbo la Jiangsu wanaendelea na kambi ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi inayofanyika katika Hospitali ya Mnazi mmoja.
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema katika kuimarisha afya za wananchi wa Zanzibar zoezi hilo la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi pamoja na matibabu litaendelea kufanyika kwa lengo la kutatua changamoto hiyo kwa akina mama hapa nchini.
Amefahamisha kuwa zoezi hilo lina lengo la kuangalia usalama wa shingo ya kizazi dhidi ya ugonjwa wa saratani na wale ambao watabainika na saratani ya shingo ya kizazi utaratibu wa kuwapatia matibabu ushaandaliwa kwa hapa nchini na ambao watatakiwa kupata matibabu zaidi nje ya nchi watatibiwa bila ya malipo yoyote.
Amewataka wanawake wote ambao wamefikia umri kuanzia miaka 18 mpaka 69 kufika Hospitali ya mnazimmoja kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi kwa kushirikiana na madaktari kutoka nchini China na wataalamu wa hapa nchini na vifaa pamoja na dawa zipo za kutosha kwa ajili ya hayo .
Kwa upande Meneja wa maradhi yasiombukiza Zanzibar Dkt Omar Mohamed Suleiman amesema uchunguzi huo unaendelea katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja ambapo pia wanatarajia kufika katika jamii ikiwemo vikosi vya SMZ, vikosi vya Muungano, pamoja na vyuo vikuu kwa lengo la kuwafikia akinamama katika maeneo hayo.
Amewasisitiza akina mama wote wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 69 ambao tayari wameshafanya tendo la ndoa kuhudhuria kufanyiwa uchunguzi huo ili kuweza kujitambua mapema na kama tayari wana viashiria vya ugonjwa huo au kuwa na ugonjwa huo kuwapatia matibabu na kuweza kuondokana na maradhi hayo.
Amefahamisha kuwa hali ya saratani ya shingo ya kizazi kidunia ni moja ya saratani iyoongoza kwa saratani kuu zinazowaathiri kinana mama wengi duniani ikifuatiwa na saratani ya matiti takribani akinamama laki mbili saabini na tano wanaugua saratani ya shingo ya kizazi kila mwaka ambapo kwa Zanzibar bado hakuna takwimu sahihi juu ya ugonjwa huo.
Amesema kutokana na ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na China zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi kwa awamu tano watawezesha kuendelea kutoa matokeo ya kujua hali halisi wa ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi hapa nchini.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa magonjwa ya Saratani kutoka Najing Hospitali ya nchini China Dkt Huaijun Zhou amesema lengo la kufanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi hapa nchini ni muendelezo wa uchunguzi wa maradhi hayo.
Amefahamisha kuwa katika awamu nne zilizofanyika waliweza kuwafanyia uchunguzi wanawake 16,500 na kati ya hao wanawake 840 waligundilika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi kwa hatua ya awali na 90 walibainika na saratani hatua kubwa na kwa awamu hii ya tano watarajia kuwafanyia uchunguzi wanawake wapatao elfu tano.