WIZARA ya Afya Zanzibar imetiliana saini mkataba na Serikali ya China ya kukabidhiwa mradi wa Hospitali ya Abdalla Mzee ya Mkoani Pemba baada ya kufanyiwa ukarabati Mkubwa na utanuzi wa Hopitali hiyo na Serikali ya China.
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema mradi huo ambao umeanza mwaka 2020 umehusisha kuongeza Majengo na kufanya matengenezo makubwa na kuongeza idadi ya vitanda kufikia 160 kutoka vitanda 80 vilivyokuwepo awali.
Amefahamisha kuwa mwanzoni Hopitali ya Abdalla Mzee ilikuwa na mita za mraba zipatazo 3260 na hivi sasa zimeongezeka zaidi na kufikia mita za mraba zipatazo elfu nane baada ya kufanyiwa utanuzi na matengenezo ambayo yamefanywa na Serikali ya China.
Amesema matengenezo na utanuzi umefanyika na kukamilika rasmi licha ya kusuwa suwa kwa matengenezo hayo kutokana na kuwepo kwa ugonjwa wa uviko 19 katika miaka ya 2020 na kupelekea kuchelewa kumalizika kwa wakati hata hivyo mwezi wa nane mwaka 2023 na Serikali ya China imekamilisha mradi huo na kuukabidhi.
Aidha ameishukuru Serikali ya China katika kuimarisha Sekta ya Afya kwenye Nyanja tofauti ikiwemo kuendeleza kwa ujenzi wa Nyumba za Madakari Mkoani pamoja na kusaidia katika masula mazima ya ugonjwa Kichocho Kisiwani Pemba.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na China hasa katika kuimarisha huduma za afya hapa nchini.
Kwa upande wake Balozi mdogo wa china aliyepo Zanzibar Zhang Zhisheng amesema China itaendelea kuisaidia Zanzibar ikiwemo sekta ya afya katika masuala mazima ya kuendelea kuleta Madaktari,mindo mbinu pamoja na dawa na vifaa tiba.
Amefahamisha kuwa kutokana na uhusiano uliokuwepo baina ya Zanzibar na China wataendeleza jitihada za kuona kuwa sekta ya afya wanaisaidia na inaendelea kukua katika visiwa vya Unguja na Pemba.