WIZARA ya Afya Zanzibar inatarajia kufanya utafiti maalum wa kitaifa wa viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza (NCD Steps Survey)

WIZARA ya Afya Zanzibar inatarajia kufanya utafiti maalum wa kitaifa wa viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza (NCD Steps Syrvey) ifikapo Septemba 9 mwaka huu ikiwa na lengo la kuandaa mikakati ya kuona maradhi hayo yanapungua.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Naibu waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh, alisema, utafiti huo utagusa jumla ya kaya 540 ambazo kwa kutumia miongozo ya kitaalamu ya kiutafiti ndizo zilizobahatika kuchaguliwa na kuwemo katika utafiti huu, kwa upande wa Pemba jumla ya kaya 180 na Unguja ni kaya 360 zitafikiwa na kuhojiwa.
Hata hivyo, alisema kuwa viongozi wakuu wa nchi wanaendelea kuchukua hatua thabiti za kiwekeza zaidi katika sekta ya afya kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.
Aidha alisema Hhali ya magonjwa yasiyoambukiza imeendelea kuwa tishio kwa ustawi wa wanadamu duniani kote. Kwa Zanzibar, hali ya magonjwa haya pia imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Alisema lengo la utafiti huo ni kuweza kutathmini hali ya Afya kuhusiana na viashiria hatarishi na mwenendo wa magonjwa yasioambukiza hapa nchini, ambapo alisema kuwa utafiti kama huu ulifanyika mwaka 2011 hapa Zanzibar na 2012 ulifanyika Tanzania Bara ambapo Zanzibar ilikuwa ndio nchi ya kwanza kufanya utafiti wa aina hii katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisema matokeo ya utafiti huo kwa Tanzania Bara, matokeo ya utafiti wa mwaka 2011 hayakuwa mazuri, ambapo vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza vilibainisha kuwa hali ya ugonjwa wa kisukari ilifikia asilimia 3.7 na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ilikuwa asilimia 33.
Aidha, viashiria hatarishi kama uzito uliokithiri ulifikia asilimia 14.3, na idadi ya watu wanaotumia sigara ndani ya kipindi cha utafiti ilikuwa asilimia 7.3, wanaotumia pombe asilimia 1.7 na watu ambao walikuwa wanajihusisha na mazoezi na kujishughulisha kwa kiwango kidogo kuliko inavyopaswa walikuwa asilimia 17.6. Utafiti ulionesha kwamba asilimia 97.9 ya watu walikuwa hawali mbogamboga na matunda kwa kiwango stahiki.
“Kwa sasa hali inaweza kuwa na taswira tofauti na ndio sababu ya msingi ya kufanya tena utafiti huu” alisema.
Aidha alisema hayua hiyo ni sehemu ya mpango wa wizara katika kuimarisha huduma za afya hasa ukizingatia kuwa maradhi yasiyoambukiza yakiwemo kisukari, shindikizo la damu, saratani, kinywa na meno yamekuwa yakiongoza kwa idadi ya vifo.
Hivyo, aliwaomba waandishi wa habari kuwajuilisha wananchi kwamba utafiti huu wa kitaifa wa viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs steps survey) unafanyika kwa pamoja Tanzania Bara na Zanzibar.
Nae, Meneja Kitengo cha Maradhi yasiyoambukiza Dk. Omar Mohamed Suleiman, alisema, zoezi hilo litafanyika kitaalamu ambapo miongoni mwa masuala yatakayoulizwa ni hali ya matumizi ya vyakula pamoja na vinywaji.
Hivyo, aliwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na wizara ya afya ili kuona magonjwa hayo yanakuwa historia nchini
Loading