Wizara ya Afya Zanzibar imesema Waste X project umewazezesha vijana wengi kujiajiri na kuweka mazingira kuwa safi

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema mradi wa kuzisarifu taka kuzigeuza kuwa thamani yaani Waste X project umewazezesha vijana wengi kujiajiri na kuweka mazingira kuwa safi pamoja kuweza kujitengenezea kipato na kufanikisha maisha yao.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt Salim Slim katika mkutano wa kufunga mradi wa Waste X Project ambao ulifanya kazi zake kwa kipindi cha mwaka mmoja na vikundi 42 hapa nchini vilikuwa wanufaika wa maradi huo.

Amefahamisha kuwa Serikali kupitia washirika wa maendeleo wakiwemo Unicef, UNDP, KOICA wameweza kushirikiana kuwapatia taaluma wanavikundi katika visiwa vya Unguja na Pemba za kuzisarifu taka kuwa za thamani na kuweza kufanya mambo mbali mbali kama vile mkaaa, mbolea, meza na vifaa vya kufanyia usafi.

Amewataka wanufaika wa mradi huo kuendelea kutumia taaluma na fursa walizozipata za kugeuza taka kuwa thamani na kuwa wabunifu wa mambo mbali mbali ya kuwapatia kipato sambamba na kuendelea kuyatunza mazingira ili kuweza kuondokana na maradhi katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Kwa upande wa Mkurugenzi Uratibu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Zainab Khamis Kibwana amesema kuwa muongozo wa kitaifa unasisitiza usafi wa mazingira na kuimarisha Afya ya jamii katika maeneo ya ngazi ya miji na vijiji.

Amesema katika suala la mazingira kilio kikubwa lipo katika uhifadhi wa taka na kuzisarifu taka kuwa fursa hivyo, kupitia mradi wa Waste X project utasaidia kutekeleza kuzisarifu taka kuwa thamani na kuyatunza mazingira kupitia vikundi mbali mbali hapa nchini.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa Chakechake Pemba Maulid Mwalim Ali amesema lengo kubwa la mradi huo ni kupiga vita masuala ya uchafu ili kuweza kuishi katika mazingira safi na salama amesisitiza kuendelea kuviimarisha vikundi hivyo na kuendelea kuleta faida kubwa kwa jamii.

Nae Meneja wa Kitengo cha Afya ya Mazingira Mlenge Hissan Mlenge amesema mradi huo umeweza kuleta mafanikio makubwa kwa wanavikundi mbali mbali hapa nchini ambapo wametengeneza bidhaa mbali mbali kupitia taka ngumu pia wanavikundi wametembelea Tanzania bara kwenda kujifunza zaidi.

Amefahamisha kuwa kitengo cha Afya na Mazingira kitaendelea kushirikiana na wanavikundi hao katika kuimarisha afya ya mazingira kwa kuleta mabadiliko hapa nchini pamoja na kuwapatia taaluma Zaidi.

Mmoja wanakikundi Fatma Maulid Shomar kutoka Kwahani amesema wameweza kupata mafanikio makubwa katika kukabiliana na kazi zao kupitia Kitengo cha Afya na Mazingira na wamejifunza sehemu tofauti na sasa wanafanya shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.

Loading