Hospitali ya Mnazi mmoja Kufanyiwa ukarabati kupitia mradi wa BADEA

Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema Hospitali ya Mnazimmoja inatarajiwa kufanyiwa ukarabati na utanuzi mkubwa kupitia mradi wa BADEA.

Ujenzi wa Hopitali ya Mnazimmoja unatarajiwa kuanza mwezi wa April 2024 ambapo mwezi wa Januari itatangazwa tenda ya ujenzi huo ambao utachukua kipindi cha mwaka mmoja hadi kumalizika kwake ambao utahusisha Hospitali ya mnazimmoja, mwmbeladu na kidongochekundu.

Waziri Mazrui ameyaeleza hayo huko Hospitali ya Mnazimmoja wakati alipozindua Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Mnazimmoja ambapo alisema nia ya kuifanyia ukarabati na utanuzi ni kuifanya Hospitali hiyo kuwa ya rufaa kutokana na kuwa itatoa huduma za kibingwa na itaweza kupunguza msongamano.

Amefahamisha kuwa ili kuifanya Hospitali ya Mnazimmoja kuwa ya Rufaa Serikali kupitia Wizara ya Afya tayari imeshajenga Hospitali kumi za Wilaya na moja ya Mkoa na itaendelea kujenga   hospitali za Mikoa yote Unguja na Pemba sambamba na kuimarisha huduma za afya ya msingi kwa lengo la kuimarisha huduma za afya hapa nchini.

Ameitaka bodi hiyo ya ushauri ya hospitali ya Mnazimmoja kusimamia vyema miradi yote inayotekelezwa kwenye hospitali hiyo iweze kukamilika kwa wakati na lengo la kuimarisha huduma za Afya liweze kufikiwa kwa ufanisi mkubwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Mnazimmoja Dkt Rukia Rajab Bakari amesema watahakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano ili kufikia malengo ya kuimarisha huduma za afya hapa nchini.

Amesema wananchi wengi wanaofika Hospitali ya mnazimmoja kwa  kupata huduma na kiioo kikubwa kwa wananchi wa Zanzibar  hivyo wataendeleza na kusimamia vyema kuona kuwa huduma zinazotolewa zinakuwa zenye ubora.

Nae mwenyekiti aliyemaliza muda wake katika bodi hiyo Dkt Abdulwakil Idrisa abdulwakil amesema dhamira kuu ya Hospitali ya Mnazimmoja ni kutoa huduma bora za afya na ustawi wa zenye kiwango cha juu.

Amefahamisha kuwa wataendelea kushirikiana na Bodi mpya kwa lengo kuimarisha huduma na kusimamia mambo yote katika hospitali hiyo ili wananchi wapate huduma zenye ubora.

Loading