Wizara ya Afya Zanzibar imesema itaendelea kushirikiana na Mashirika ya kimataifa kutokomeza Malaria Zanziabr

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema itaendelea kushirikiana na Mashirika ya kimataifa na wadau wengine kuhakikisha kuwa maradhi ya Malaria yanaondoka hapa nchini.

Akifungua Mkutano wa siku moja wa Mpango Kazi kwa mwaka 2025 uliowashirikisha Wadau na Mashirika ya Kimataifa   Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Wizara  ya Afya Zanzibar  Dkt Salim Slim amesema jitihada zinafanyika kwa wananchi juu ya kujikinga na maradhi hayo.

Amesema katika kipindi cha miaka kumi na saba mpaka ishirini nyuma Zanzibar iliweza kufanya mambo makubwa ya kudhibiti maradhi ya Malaria kwa kiasi kikubwa, hata hivyo katika kipindi cha hivi karibuni kulitokea mripuko wa maradhi hayo yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema kutokana na hali hiyo Wizara ya Afya kwa kushirikana na Mashirika ya Kimataifa na wadau wengine waliweza kufanya kazi kubwa ya kudhibiti maradhi hayo ambapo kwa sasa maradhi hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa hapa nchini na kuwataka wannchi kutumia kinga dhidi ya maradhi hayo.

Amefahamisha kuwa lengo la Serikali ni la kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapatiwa kinga dhidi ya Malaria na anaitumia ipasavyo kwa lengo la kuondokana pamoja na kujikinga na Malaria hapa nchini.

Kwa upande wa Meneja wa Programu ya kumaliza Malaria Zanzibar Shija Joseph Shija amesema lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau wanaosaidia mapambano dhidi ya malaria na kuandaa mpango kazi wa mwaka mmoja na kuwasilisha na kuweza kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya matumizi.

Amelipongeza Shirika la PMI na wadau wengine  kwa kusaidia mapambano dhidi ya Malaria na kuhakikisha kuwa wanapata fedha za kutekeleza kazi mbali mbali ambazo wamejipangia kwa lengo la kuondokana na maradhi hayo.

Amefahamisha kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa ya kumaliza malaria hapa nchini licha ya kutokea mripuko wa maradhi katika siku za hivi karibuni ambapo jitihada zilifanyika ya kuyaondosha maradhi hayo na kwa sasa maradhi hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Amewasisitiza wananchi kuendelea kukubali kazi zinazofanywa na Programu ya kumaliza Malaria kwa jamii na kuzingatia mbinu ya kujikinga na maradhi hayo ikiwemo kulala kwenye Chandarua, upigaji dawa majumbani  pamoja kuweka usafi wa Mazingira.

Kwa upande wake wake Katibu Mtendaji wa kupambana na maradhi ya Malaria Kifua kikuu na Ukimwi katika ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Dkt Abdalla Suleiman amesema  kazi kubwa wanayoifanya ni kusaidia katika kutafuta fedha, wataalamu ili kuweza kuendeleza kazi kwa mujibu wa muda uliopangwa.

Amefahamisha kuwa katika kutekeleza kazi hizo wanapa fedha katika mradi wa  mfuko wa fedha wa Dunia Global Fund  na tayari kwa mwaka huu 2024 wamesaini mkataba kwa mujibu wa mahitaji ya programu hizo.

Kwa upande wa Mkurugenzi anaeshughulikia Masuala ya Afya USAID amesema wameweza kusaidia nchi mbali mbali ikiwemo Tanzania, Kenya Uganda katika mapambano dhidi ya Malaria na kupatikana kwa mafanikio makubwa.

Amesema wataendeleza jitida zao kwa Zanzibar  katika program ya kumaliza Malaria  ili kuweza kundokana na maradhi hayo.

Loading