Wizara ya Afya Zanzibar imesema itaanza kuhamisha huduma za uzazi katika Hospitali ya Mnazi mmoja ili kuweza kupisha ujenzi, ukarabati na utanuzi wa Hospitali hiyo unaotarajiwa kuanza mwezi wa sita mwaka huu.
Akitoa Taarifa kwa wananchi Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh amesema kutokana na kuanza kwa taratibu za utanuzi na ujenzi wa Hospitali ya Mnazimmoja huduma za uzazi zitaendelea kutolewa katika ngazi tofauti za utoaji wa huduma.
Amefahamisha kuwa huduma hizo zitatolewa katika vituo vya afya, Hospitali za Wilaya,na Hospitali ya Rufaa Mkoa Mjini Magharibi Lumumba ambayo ndiyo itakayotoa huduma za rufaa kwa kipindi chote ambacho Hospitali ya rufaa ya mnazi Mmoja itakapokuwa katika matengenezo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Amour Suleiman Mohamed amesema wameandaa utaratibu maalumu wa kuwahamisha wazazi kutoka Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja kwenda kupata huduma katika hospitali ya Mkoa Lumumba, Hospitali za Wilaya bila ya kuleta athari yoyote.
Amefahamisha kuwa Wizara ya Afya itahakikisha inapeleka Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Mkoa na Wilaya ili kuweza kutoa huduma kwa ufanisi.