Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Pharm Access kuimarisha huduma za Afya Zanzibar

WAZIRI wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema wataendelea kushirikiana na shirika la Pharm Access ili kuona wanaendelea kuwapatia huduma wananchi za afya zinaimarika nchini na kuendelea kutolewa kwa wakati.

Akizungumza katika uzinduzi wa vikundi vya wagonjwa wanaishi na magonjwa yasiyoambukizwa (NCD) katika jamii ikiwemo ya presha na kisukari hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa skuli ya Bumbwini.

Alisema, magonjwa yasiyoambukiza kwa sasa ni tishio Zanzibar ambao kwa sasa serikali kwa kushirikiana na wadai mbalimbali wameweka mipango madhubuti ili kuona wanapambana na maradhi hayo..

Alisema, wameweka mikakati ya kuimarisha vituo vya afya ikiwemo kuwapatia elimu wahudumu wa afya katika jamii (CHV) ili kuondelea kutoa huduma za afya kwa wanajamii zilizokuwa bora zaidi.

Alisema, kuzinduliwa wa mpango huo, utaweka mkakati wa kuimarisha afya kwenye jamii ikiwemo, kuziboresha Zahanati hadi Dispensary lengo ni kuimarisha afya ya msingi kuanzia kwenye jamii yenyewe.

Mkurugenzi mkaazi wa shirika la Pharm Access, Dk. Heri Marwa, shirika lao limekuwa likifanya kazi katika nchi nne ikiwemo,  Ghana, Kenya, Naigeria na Tanzania na lengo kuu ni upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Alisema,  kutokana na changamoto zinazowakabaili wagonjwa wenye maradhi hayo, shirika lao limeona ni vyema kuwarahisishia upatikanaji wa huduma za afya katika wilaya zao.

Alisema ni muhimu kuwa na mikakati ya kudhibiti magonjwa hayo ili kuweza kuondosha gharama za kujitibu magonjwa hayo kwa serikali na familia.

Sambamba na hayo, alisema, shirika lao lipo tayari kushirikiana na serikali ili kuhakikisha mfumo huo wa kutoa huduma za magonjwa hayo ziweze kufika katika wilaya 11 za Zanzibar ili ziweze kufikiwa na huduma.

Mapema, Mkuu wa kitengo wa maradhi yasiyoambukiza, Dk. Omar Mohammed Suleiman, alisema, kupitia wafadhili wa shirika la  Pharm Access imerahisisha kujua wagonjwa wao sambamba na kuwapatia huduma zilizokuwa bora kwa wagonjwa wa kisukari na presha.

Aidha alisema, mradi huo kwa sasa upo katika wilaya mbili za mkoa wa kaskazini lengo lao hapo baadae kuifikia jamii yote ya Zanzibar ili kuona wanapambana na magonjwa hayo.

Akizungumza juu ya mfumo huo ulioanzishwa, daktari kutoka kituo cha Afya Bumbwini Misifuji, Dk. Aisha Wadi Ame, alisema, huduma hizo zimesaidia kuwapunguzia masafa wagonjwa hao ambapo wamekuwa wakipata huduma kwa urahisi pamoja na upatikanaji wa dawa kwa urahisi kwa wagonjwa wao.

Alisema, kupitia vikundi hivyo, wameweza kuwapatia elimu ya afya ya presha na kisukari ambapo taarifa ya vipimo vyao vimekuwa vikiunganishwa kwenye mfumo na daktari jambo ambalo limesaidia hufuatilia maendeleo ya wagonjwa bila ya usumbufu.

Akitoa ushuhuda wa upatikanaji wa huduma zinazotolewa, Jafari Iyombwe Haji, alishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Wizara ya ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Pharm Access kwa kuwapelekea huduma katika kijiji chao kwani imewarahisishia upatikanaji wa huduma ambapo awali walikuwa wakipata usumbufu.

Aidha alifahamisha kuwa sasa wamekuwa wakipata huduma hizo kwa urahisi na kwa ukaribu wa hali ya juu ambapo madaktari wamekuwa wakiwapatia huduma stahiki na kwa wakati.

Loading