WIZARA ya Afya imesema itaendelea kushirikiana na Serikali ya China katika kuimarisha afya za wananchi wake

WIZARA ya Afya imesema itaendelea kushirikiana na Serikali ya China katika kuimarisha afya za wananchi wake.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya, Dk.Salim Slim, alipokuwa akifungua zoezi la upimaji wa afya kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), zoezi lililoendeshwa na timu ya madaktari kutoka China.

Alisema, upimaji wa afya kwa watumishi wa umma ni jambo bora na muhimu kwani litasaidia hata kuongeza tija katika taasisi baada ya kutambua afya zao kwenye uwajibikaji wa majukumu.

Aidha, alisema, kuwa kwa kutambua afya za wafanyakazi pita kutamuwezesha mwajiri kuongeza ufanisi hasa katika utekelezaji wa majukumu mbali mbali ya kiutendaji kwenye maeneo yao ya kazi.

“Kama mtumishi atakuwa na afya njema basi atasaidia kuongeza uzalishaji katika taasisi hivyo wafanyakazi wanatakiwa kupima afya zao ili kuongeza ufanisi”.

Naye Mkuu wa Madakari kutoka China, Profesa Jiang Guoqing, alisema, lengo la upimaji afya huo ni katika jitihada za kuwasaidia watumishi kujenga tabia ya kutambua afya zao mara kwa mara.

“Leo tumekuja kufanya uchunguzi wa kiafya hapa ZAA kwa kutambua umuhimu mmkubwa wa taasisi hiyo yenye kuhudumia watu wengi”.

“Wafanyakazi viwanja vya ndege ni watu muhimu kutokana na majukumu yao ya kuhudia kitaifa na kimataifa, huduma za kiafya ni jambo la msingi kwao”.

Aidha, aliishukuru Wizara ya Afya na Serikali kwa namna zinavyotoa ushirikiano mkubwa madaktari wa Kichina wanapofika Zanzibar kwa ajili ya kutoa huduma mbali mbali.

Mapema, Mkurugenzi Viwanja, Rob Williams, alisema, zoezi hilo litawasaidia wafanyakazi kutambua nini wafanye na kipi wasifanye ili kuwa na afya njema na kuendelea kuleta tija katika maeneo yao ya kazi.

“Wafanyakazi wanatakiwa pia kufanya mazoezi ili kua na afya njema itakayomuweka kwenye uwajibikaji mzuri”, alisema, Williams.

Naye Ofisa Dhamana Huduma za Afya Uwanja wa Ndege, Nassor Hamad Said, alisema,
lengo la zoezi hilo ni kutoa fursa kwa wafanyakazi kupima afya zao kwa ajili ya kuleta maendeleo.

Nao wafanyakazi hao walielezea kufurahia kupata fursa hiyo kwani inawapa nafasi ya kutambua afya zao na kufanya kazi kwa bidii na kuongeza tija katika maeneo yao ya kazi.

Loading