Wizara ya Afya Zanzibar imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali ya China katika kutoa huduma mbali mbali za Afya

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali ya China katika kutoa huduma mbali mbali za Afya ikiwemo kuwafanyia uchunguzi wa maradhi ya saratani shingo ya kizazi.

Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui ameyaeleza hayo   katika Mkutano wa kupokea ripoti ya uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya kizazi iliyofanywa na madaktari kutoka nchini China, Hospitali ya Mnazimmoja,  na Kitengo cha Maradhi yasiombukiza iliofanyika tarehe 4 mpaka 28 ya mwezi wa 11.

Amesema kwa awamu hii ya tano watu elfu mbili na mia nane wamefanikiwa kufanyiwa uchunguzi ambapo ni chini ya lengo lilokusudiwa iliyochangiwa na hali ya mvua na mafauriko katika maeneo mbali mbali hapa nchini.

Waziri Mazrui alifahamisha kuwa wamejipanga kwa zoezi la awamu ijayo kwa kuwafanyia uchunguzi watu wengi zaidi katika visiwa vya Unguja na Pemba na watakaogundulika watapatiwa matibabu ili kuweza kupunguza maradhi hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Amour Suleiman Mohamed amesema mbali na uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi pia waliweza kuchunguza na maradhi mengine yakiwemo magonjwa ya kujamiina na waliogundulika na maradhi hayo walipatiwa matibabu.

Kwa upande wake Meneja wa Kitengo cha Maradhi yasiombukiza Zanzibar Dkt Omar Mohammed Suleiman amesema kuwa zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi litahusisha akinamama wapatao 34,000 Unguja na Pemba na linatarajiwa kumalizika mwakani.

Amefahamisha kuwa hadi kufikia sasa jumla ya wanawake 19,432 tayari wameshafanyiwa uchunguzi katika awamu tofauti ambapo kwa awamu hii ya tano jumla ya wanawake 2800 sawa na asilimia 56 wamechunguzwa ambapo ni chini ya lengo la wanawake 5000.

Amesema jumla ya wanawake 77 wamegundulika na saratani ya shingo ya kizazi ambapo wanawake 59 wamethibitishwa kuwa na saratani hatua ya awali na wanawake 18 wamegundulika kuwa na saratani hatua kubwa wamepatiwa matibabu Hospitali ya Mnazimmoja na wangine wamepekwa Ocean Road kwa matibabu zaidi.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa magonjwa ya Saratani kutoka Najing Hospitali ya nchini China Dkt Huaijun Zhou amesema lengo la kufanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi hapa nchini ni muendelezo wa uchunguzi wa maradhi hayo.

Amesema kutokana na ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na China wataendelea kufanya  zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi kwa na   kuendelea kutoa matokeo na yatawezesha  kujua hali halisi wa ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi hapa Zanzibar.

Loading