Wizara ya Afya imepokea msaada wa vifaa Tiba kwa Hospital ya Kivunge

WIZARA ya afya Zanzibar imepokea msaada wa vifaa tiba kutoka Serikali wa watu wa China Jimbo ya Jiangsu vyenye thamani ya Zaidi ya milioni mia tatu.

Akipokea vifaa hivyo huko Hospitali Kivunge Mkurugenzi Tiba Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Msafiri Marijani amesema vifaa hivyo ni pamoja na vifaa vya upasuaji vya kutumia   tundu ndogo kwa kutumia video na vifaa vya kutumia tiba mtandao.

Amesema upasuaji wa kutumia video na tundu ndogo unamuwezesha mgonjwa kupasuliwa sehemu ndogo na kupata maumivu kidogo na tiba mtandao itasaidia kuwasiliana na madaktari waliokuwepo hospitali ya Jiangsu na madaktari wa Kivunge kwa kuelekezwa matibabu mbali mbali katika hospitali hiyo.

Amefahamisha kuwa kusaidiwa kwa vifaa hivyo vitasadia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma za afya hapa nchini ambapo wameweza kuanzisha kituo maalumu cha upasuaji wa video wa kutumia tundu ndogo ambao upasuaji wake mgonjwa anakuwa uponaji wake unakuwa wa haraka.

Kwa upande wake muakilishi kutoka Hospitali ya Jimbo la Jiangsu Profesa Xiuqin Wang   amesema wameona ipo haja ya kusaidia vifaa hivyo katika Hospitali ya Kivunge ili kuwezesha kutoa huduma kwa urahisi kwa wagonjwa.

Amesema Hospitali ya Jimbo la Jiangsu wataendeleza ushirikiano wao na Zanzibar katika sekta ya afya na hiyo kutokana na uhusiano uliopo ni wa muda mrefu na  ambao lengo kubwa ni kuwasaidia wananchi wa Zanzibar wapate matibabu bila ya usumbufu wowote.

Kwa upande wake msaidizi daktari  dhamana wa Hospitali ya Wilaya Kivunge Tamim Hamad Said ameshukuru kusaidiwa msaada huo ambao utawasaidia madaktari wa hospitali hiyo kufanya kazi zao kwa urahisi na kwa ufanisi mkubwa.

Amesema pia watafaidika kupata ujuzi Zaidi kutoka kwa madaktari mbali mbali waliopo katika hospitali ya Jimbo la Jiangsu kwa njia ya mtandao na kuweza kutoa huduma zilizobora katika hospitali hiyo.

Uhusiano wa Hospitali ya Jiangsu China ni makubwa kutokana na kuwa makubaliano yaliyotiwa saini mwaka 2022 baina ya hospitali ya Kivunge na Chakechake Pemba na wanawezeshwa katika kusaidia katika huduma mbali mbali za Afya.

Loading