Rais Mwinyi amewakumbusha wauguzi na watumishi wa sekta ya afya kuisaidia serikali kuleta Maendeleo

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewakumbusha wauguzi na watumishi wote wa sekta ya afya kuendelea kuisaidia serikali katika kuhakikisha inatekeleza malengo yake ya kuwapatia huduma bora za afya wananchi wa Zanzibar bila ya ubaguzi.

Dk.Mwinyi alieleza hayo katika kilele cha siku ya wauguzi duniani iliyofanyika katika ukumbi wa Shekh Idrissa Abdul Wakili Kikwajuni.

Alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa Shabaha ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 katika kutoa huduma za afya na mipango mikuu ya sekta ya Afya hapa Zanzibar.

Aidha alisema serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha huduma za afya nchini zinaimarishwa ili ziweze kuwa bora zaidi.

Rais Mwinyi alibainisha kuwa serikali imefanya jitihada kubwa katika kuongeza bajeti ya sekta ya afya, kujenga miundombinu ya afya ikiwemo ujenzi wa hospitali za wilaya na mkoa pamoja na kuzifanyia matengenezo makubwa hospitali na vituo vya afya Unguja na Pemba.

Vile vile, alisema wanaendelea na juhudi katika ununuzi wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi na vya tiba sambamba na kuongeza nafasi za ajira kwa madaktari na watumishi wengine kwa sekta ya afya na kuendeleza mpango wa mafunzo ili kuwajengea uwezo watumishi wa sekta hiyo kwa lengo la kuongeza ufanisi.

Alifurahishwa na maendeleo makubwa katika kada hiyo kwa kuwa na maprofesa wengi wa uuguzi na ukunga hivyo ni mategemeo yake kuwa huduma zitatolewa kwa weledi zaidi.

Rais Mwinyi aliwasihi wauguzi wote kwa jumla kuwa na moyo wa huruma, kutumia lugha nzuri na kufata maadili ya taaluma yao wakati wote wanapotoa huduma kwa wagonjwa.

Akizungumzia kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wauguzi duniani inayosema “WAUGUZI WETU NI MUSTAKABALI WETU” kwani kauli mbiu hiyo imechaguliwa ili kuonesha nafasi muhimu ya mchango unaotolewa na wauguzi katika kuleta ustawi wa maisha katika jamii duniani kote.

Alisema hapana shaka kwamba, bila ya wauguzi kutekeleza vyema majukumu yao, afya ya jamii na maisha yao kwa jumla yako mashakani.

Hivyo, alitumia fursa hiyo kuwahimiza kuipa umuhimu na mazingatio kaulimbiu hiyo kwa kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wagonjwa vizuri kwa kuwapa msaada unaohitajika na kuhakikisha wanapata huduma bora katika hospitali zote na vituo vya afya mijini na vijijini.

Aliwapongeza wauguzi ambao wanafanya kazi vizuri kwa uadilifu na kujituma usiku na mchana bila ya kuchoka ya kuhudumia wagonjwa na kuwasihi kuendelea na kuwa na moyo huo ili kufanikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Serikali yenu pamoja na wananchi wa Zanzibar tunaridhishwa na kazi nzuri mnayoifanya na walio wengi katika kutekeleza majukumu yenu katika mazingira yenye changamoto nyingi,” alisema.

Dk. Mwinyi aliwahimiza kuwa na ushirikiano na kada nyengine wakiwemo, madakatari, wafamasia, wachunguzi, wahudumu ili wananchi wapate huduma zilizobora unaotakiwa.

Hata hivyo, akizungumzia changamoto zinazowakabili katika kazi yao ikiwemo uhaba wa wauguzi katika ngazi alisema serikali kupitia Wizara ya Afya imeanza kuajiri wauguzi na wataendelea kufanya hivyo katika mwaka ujao wa fedha.

Alitumia nafasi hiyo kuwahimiza kuongeza bidii ya kufanya kazi kwa moyo, uzalendo na kujituma wakati serikali inaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto za kikazi zinazoikabili kada ya uuguzi.

Alisema amefarajika kusikia kuwa Baraza la Wauguzi na Wakunga wa Zanzibar wamejiandaa kukabiliana na tatizo la maadili kwa kutoa vitabu vitakavyokabidhiwa kwao kama muongozo katika utekelezaji wa kazi zenu.

Hivyo, aliwataka viongozi wote wa wauguzi na viongozi wa Wizara ya Afya kuhakikisha wanafatilia utekelezaji wa miongozo hiyo ili hadhi na heshima ya taaluma ya uuguzi iendelee kudumu.

Sambamba na hayo aliiagiza Wizara ya Afya kuhakikisha inatoa fursa za masomo za ndani na nje ya nchi kwa kada hiyo na kuhakikisha wanayatafutia ufumbuzi wa haraka changamoto ya kukosa posho ya dhamana na sare kwa watumishi hao.

Akimkaribisha Rais Mwinyi, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh, alisema dhana na azma anayoitaka Rais Mwinyi inaaza kufikiwa katika kutoa huduma bora kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema Rais Mwinyi ameinua huduma za afya kwa wananchi wa Zanzibar ili kuona wananchi hawapati usumbufu katika kupata huduma zote za afya ikiwemo vipimo na matibabu bora katika hospitali na vituo vyote vya afya Unguja na Pemba.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya za Wauguzi Zanzibar (ZANA), Dk. Rukia Rajab, alisema pamoja na kada hiyo kukabiliwa na changamoto mbalimbali lakini zisiwakatishe tamaa bali kuzibadilisha na kuwa fursa na chachu ya kuendelea kufanya kazi na kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa kwa kuwahudumia wagonjwa wenye uhitaji na jamii kwa ujumla.

Aliwataka wauguzi na wakunga wa Zanzibar kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wagonjwa kwa kuzingatia maadili na utendaji uliotukuka ili kuimarisha afya za jamii na kuisaidia serikali katika kufikia malengo endelevu ifikapo mwaka 2030.

“Huduma tunazozitoa kwa wagonjwa ni wito na dhamana tuliyopewa na Mwenyezimungu tukumbuke kuwa kazi zetu zina faida kubwa hapa duniani na akhera na tufanyeni kazi kwa bidii na tukifanya mzaha basi tutahukumiwa hapa duniani na kesho akhera,” alisisitiza.

Aliwasisitiza wauguzi kubadilika ili waweze kutajika vizuri katika jamii na kurudi katika majukumu yao maadili sambamba na kufuata miongozo na sheria inavyowaelekeza.

Akisoma risala kwa niaba ya wauguzi wenzake muunguzi Said Kheir Hamad, alisema wauguzi wametoa mchango mkubwa duniani kupunguza vifo vya watoto wachanga, malaria, ukimwi na maradhi mengine.

Hata hivyo, alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uchache wa wauguzi kulingana na wagonjwa wanaowahudumia kwani hakuna viwango sawa unaokidhi viwango vya kimataifa, uhaba wa wauguzi bingwa katika fani mbalimbali ikiwemo maradhi ya saratanimifumo ya fahamu na ubongo marandhi ya mifupa na maradhi mengine.

Walipongeza Rais Mwinyi na serikali yake kwa kurodhiroa na kuwateuliwa Mkurugenzi wa ukunga katika ngazi ya wizara na kuhakikisha kada ya wauguzi inaendelea kuimarika.

Waliahidi kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa kufuata muongozo, maadili,sheria na kanuni zilizopo ili kuimarisha huduma kwa wagonjwa na wenye maahitaji na kuwaasa wale wachache wasiofata maadili ya uuguzi kuacha tabia hiyo na badala yake kufuata maadili na miongozo ya kazi yao.

Loading