Wizara ya Afya imefanya mazungumzo na kuagana na Balozi wa Norway ambae amemaliza muda wake nchini Tanzania

WIZARA Afya Zanzibar imesema itaendeleza ushirikiano na Norway katika kuimarisha Sekta ya Afya na wananchi wapate huduma zenye ubora.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui alipofanya mazungumzo na Balozi wa Norway nchini Tanzania Elizabeth Jacobsen ambae amefika ofisini kwake kuaga kwa kumaliza muda wake.

Waziri Mazrui amefahamisha Norway imeweza kuisadia Sekta ya afya katika Nyanja mbali mbali ikiwemo ujenzi wa hospitali wa wagonjwa wa akili, Hospitali ya Mnazimmoja mama na mtoto pamoja na kujenga Maabara ya kujifunzia kwa vitendo ambayo ujenzi wake utaanza hivi karibuni katika maeneo ya Lumumba.

Amesema kupitia chuo kikuu cha Hookland cha nchini Norway itajenga Hospitali ya magonjwa ya Moyo ambayo itawezesha kutoa huduma za maradhi hayo hapa nchini ambapo alimuelezea Balozi huyo kwa sasa huduma hizo wanapata Tanzania Bara na nnje ya nchi.

Aidha amesifu jitihada kubwa zinazofanywa na Norway katika kuimarisha sekta ya Afya na kumuomba kuendeleza misaada yao na uhusiano uliopo  baina ya nchi hizo.

Kwa upande wake Balozi wa Norway nchini Tanzania Elizabeth Jacobsen amesema wataendeleza ushirikiano wao na Zanzibar katika kusaidia sekta mbali mbali ikiwemo Afya.

Amesema atahakikisha Serikali ya Norway inaendelea   kutekeleza misaada yao kwa Zanzibar katika kuinua huduma za Afya na mafunzo kwa wafanyakazi wake.

Loading