Wizara ya Afya imepokea msaada wa vifaa mawasiliano ya internet kutoka Save the Children

WIZARA ya Afya Zanzibar imepokea msaada wa vifaa vya mawasiliano ya Internet kutoka Shirika la save the Children vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 26.

Vifaa hivyo vitatumika katika vituo vya mkono kwa mkono one stop centre  kwa Unguja na Pemba kwa ajili ya kuweka kumbu kumbu za kesi mbali mbali wanazopokea vituoni mwao.

Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Amour Suleiman Mohamed amesema  vifaa hivyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha utendaji wa kazi za vituo hivyo pamoja na kuweka taarifa za wahanga wa matukio ya udhalilishaji.

Amefahamisha kuwa vitondo vya udhalilishaji vinatokea katika jamii, hivyo ni vyema watendaji na madaktari kufanya jitihada za makusudi kuzishughulikia kesi hizo mapema ili muhanga wa kesi hizo asiweze kuathirika zaidi.

Amelitaka Shirika la save children kuendeleza jitihada zake za kusaidia sekta ya afya hasa katika kuwajengea uwezo wafanyakazi wake vifaa na masuala mazima ya lishe ili kuwa na watoto wenye afya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la save the Children Angela Kauleni amesema kutokana  na masuala ya udhalilishaji na ukatili kwa watoto yanatokea katika jamii na watahakikisha kuwa masuala hayo yanaondoka kwa kufanya jitihada mbali mbali ikiwemo elimu kwa jamii.

Amefahamisha kuwa katika kuondosha tatizo hilo wameweza kuunda mabaraza ya watoto katika jamii ambapo wanaweza kujisemea matatizo yao na wanafanya kazi kwa karibu na viongozi wa dini na walimu katika maskuli mbali mbali lengo ni kuondosha matatizo hayo.

Amesema katika masuala ya ukatili wa watoto haliwezi kuvumiliwa na watahakikisha haki za watoto zinapatikana kwa kuwa na mashirikiano na watu mbali mbali na ikiwemo wazazi katika  katika malezi ya watoto na lishe.

Nae Mkurugenzi Tiba Wizara ya Dkt Msafiri Marijani amesema bado masuala ya uwekaji wa taarifa hasa katika masuala ya udhalilishaji halipo vizuri na kupatikana kwa msaada huo utafanikisha utunzaji wa taarifa.

Katika makibidhano hayo ya vifaa save the children imetoa namba ambayo itatumika kupiga bure na mtu yoyote anaweza  kuelezea matukio yanayotokea ya udhalilishaji na ukatili na kuweza kufanyiwa kazi haraka.

Shirika la save the Children ni Shirika linaloshughulikia masuala ya watoto  Tanzania na hapa Zanzibar shirika hilo lilianza kufanya kazi zake tangu mwaka 1986 na dira yao kubwa ni kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata kikamilifu haki za kuishi.

Loading