Waziri wa Afya akutana na Ujumbe wa GHC Hospitals kutoka India

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya Zanzibar, imesema itaendeleza jitihada zake za kuimarisha huduma za maradhi ya moyo hapa nchini kwa kuleta madaktari bingwa wa magonjwa hayo kutoka nchi mbali mbali ikiwemo India ili kuweza kufanya uchunguzi na kuwapatia matibabu wagonjwa wenye maradhi hayo.Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui alipofanya mazungumzo na ujumbe kutoka GHC Hospitals za nchini India huko ofisini kwake walipofika kujitambulisha.

Amesema magonjwa ya moyo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku hapa nchini hivyo ujio wa madaktari hao kutoka nchini India utasadia katika utoaji wa huduma za magonjwa ya moyo pamoja na kuwafanyia uchunguzi, Na kuwapatia matibabu sambamba na wataalamu wa Zanzibar kwenda kujifunza katika hospitali za India ili kuweza kutoa huduma kwa ufanisi.

Amefahamisha katika kufanikisha utoaji wa huduma hizo ambazo zitafanyika kwa mashirikiano makubwa na GHC Hospitals na Wizara ya afya, watatiliana saini mkataba maalum wa mashirikiano ambao utahusisha kuja kufanya uchunguzi na utoaji wa huduma na kuwapatia mafunzo zaidi nchini India kwa wafanyakazi wanaoshughulikia wagonjwa wa moyo. Waziri Mazrui amesema kuna baadhi ya watoto wanaozaliwa moyo yao haipigi vizuri na wengine kuwa na tundu na matatizo mengine, hivyo madaktari hao watasaidia kufanya utafiti wa kina kuona chanzo cha tatizo hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti na Mkurugenzi wa GHC Hospitals dkt Zainalebedin Hamdulay amesema wataisaidia Zanzibar katika huduma za magonjwa ya moyo kwa kufanya uchunguzi wagonjwa pamoja kuwapatia matibabu na ambao watahitaji matibabu zaidi wataangalia namna ya kusaidia.Amefahamisha GHC Hospitals wanatoa huduma katika nchi mbali mbali na kuwapatia matibabu yakiwemo ya upasuaji na wamekuja Zanzibar kwa nia ya kuwasaidia wananchi ili kuweza kuwapatia huduma zenye ubora.

Loading