Waziri Mazrui azungumza na waandishi wa habari kuelekea siku ya wachangia damu Duniani

Waziri wa Afya, Mhe.Nassor Ahmed Mazrui amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchangiaji wa damu ili kupunguza maradhi na vifo vinavyotokana na upungufu wa damu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari huko Ofisini kwake Mnazi Mmoja amesema kutokana na umuhimu wa uchangiaji damu ipo haja ya wananchi kujitokeza kutoa damu kwa moyo mkunjufu ifikapo tarehe 14 Juni huko Makao Makuu ya damu salama Sebleni ili kuwachangia wagonjwa wanaohitaji huduma ya damu hospitalini kutokana na sababu moja au nyengine.

Amesema sababu kubwa zinazopelekea kuhitaji tiba ya damu ni kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, ajali au upasuaji na pia upungufu wa damu kwa watoto na watu wazima kutokana na sababu mbali mbali.

Waziri Mazrui alifahamisha kuwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama unaozingatia uchangiaji wa damu kwa hiari, umeanza mwaka 2005 kwa Zanzibar chini ya Wizara ya Afya kwa Ufadhili mkubwa wa Mfuko wa Rais wa Marekani wa kupunguza kasi za maambukizi ya UKIMWI ukiwa na lengo la kupunguza kasi ya maambukizi ya pamoja na kuziwezesha hospitali kuwa na akiba za damu za kutosha wakati wote kwa ajili ya matumizi.

Ametoa wito kwa jamii kuwa na utaratibu wa kula mlo kamili zikiwemo mboga mboga hasa kwa mama wajawazito ili kujitengenenezea afya njema yeye na mtoto na kujiwekea mazingira mazuri wakati wa kujifungua.

                                     Meneja Mipango wa Damu salama Dkt. Salama Rashid Abdalla

Kwa upande wake Meneja Mipango wa Damu salama Dkt. Salama Rashid Abdalla amesema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani Zanzibar imependekezwa kuchangia chupa za damu elfu kumi na sita kwa mwaka.

Amesema kiwango cha ukusanyaji wa damu salama kwa mwaka 2021 kilikuwa kikubwa lakini hakikukidhi mahitaji kwa wagonjwa wanaohitaji damu hizo, hivyo amewaomba wananchi wenye vigezo vya kuchangia damu kufika kwa wingi kwa ajili ya kuchangia.

                                                                             Afisa Uhusiano Damu Salama Ussi Bakar Mohamed

Nae Afisa Uhusiano Damu Salama Ussi Bakar Mohamed, akielezea vigezo vya mtu anaeweza kuchangia damu amesema ni lazima awe na Umri kati ya miaka 18 na 65, Uzito usiopungua kilo 50, Wingi wa Damu wa kutosha (Hb 90% sawa na 13.0gm/dl kwa mwanamme, Hb 85% sawa na 12.5 gm/dl kwa mwanamke).

Aliendelea kwa kusema, wingi huu wa damu utapimwa kabla kuchangia damu na pia mchangiaji hapaswi kuwa mtu mwenye maradhi endelevu kama vile Kisukari, Presha, Maradhi ya Moyo, Pumu, na Kifafa.

Siku ya Wachangiaji Damu Duniani hufanyika tarehe 14 June ya kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni

“Kuchangia damu ni kitendo cha mshikamano, tuungane tuokoe maisha”

Loading