Wizara ya Afya imeamua kuchukuwa hatua madhubuti na kuhakikisha wanaondosha changamoto zinazowakabili ili kupunguza vifo vya mama na mtoto nchini.
Hayo amesema Mkurugenzi wa Kinga na elimu ya afya Dr. Ali Said Nyanga wakati akifungua mkutano wa mwaka wa kujadili afya ya mama na mtoto huko ukumbi wa chuo cha utalii Marughubi Mjini Zanzibar.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inajenga hospitali za Wilaya na kuongeza sehemu za kujifungulia ili kuondosha msongamano wa kwenda kujufungulia Hospitali ya Mnazimmoja kwa lengo kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Amesema lengo la mkutano huo ni kujifunza mambo mbalimbali na kuandaa mikakati madhubuti itakayoongeza hamasa ya utendaji kazi pamoja na kuzuia uzembe ambao utapelekea vifo kwa mama wanapofika kujifungua hospitalini.
Aidha amesema Wizara ya afya inathamini juhudi zinazotolewa na mashirika ya afya kwa kusaidia kupitia nyanja mbalimbali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
Vilevile amewataka watendaji wabadilike katika kutoa huduma kwa kuongeza usimamizi na ukaguzi katika vituo vinavyotoa huduma ya mama na mtoto.
Nae kaimu meneja kitengo Shirikishi Afya ya mama na mtoto Dkt Farhat Jowhar Khalid amesema mkutano huo ni muhimu sana na utasaidia kutafuta njia mbadala ili kuzidhibiti vifo na kuboresha huduma ya mama na mtoto nchini.
Nae muwakilishi kutoka shirika la UNFPA Dkt Azza Said Amiin amesema Shirika lake linaunga mkono juhudi za serikali za kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kuimarisha upatikanaji wa dawa,vifaa tiba pamoja na kutoa mafunzo na kujenga uwezo kwa wafanyakazi ili kutoa huduma bora za afya ya uzazi.
Aidha ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuimarisha sekta ya afya na kuweka mazingira mazuri kwa mashirika ya umoja wa Mataifa na washirika wengine wa maendeleo yanayounga mkono juhudi za kuokoa vifo vya mama na mtoto