Wananchi wa Zanzibar wamehimizwa kujenga tabia ya Kuchunguza Afya zao mara kwa mara

WANANCHI visiwani Zanzibar wametakiwa kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya zao ikiwemo   macho ili kuweza kuondokana na athari mbali mbali ambazo zinaweza kujitokea athari katika macho.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Kinga na Elimu ya afya Zanzibar Dkt. Salim Slim huko Tumbatu katika maadhimisho siku ya uoni  duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo terehe 12 ya mwezi wa kumi kila mwaka na ujumbe wa mwaka huu ni “penda macho yako ukiwa kazini”

Amesema iwapo wananchi watakuwa na tabia ya kufanya uchunguzi wa macho   mara utasaidia kubaini mapema viashiria vinavyoweza kusababisha magonjwa sabambamba na kupatiwa matibabu stahiki na kwa  wakati na kuepukana matatizo makubwa ikiwemo upofu.

Amewataka wananchi kufika katika vituo vya afya viliyo karibu nao kwa ajili ya hatua zaidi wanapohisi mabadiliko yoyote kwenye macho ikiwemo macho kuuma, kuwasha au kutokuona vizuri.

Dkt. Slim amebainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia wizara ya afya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kusogeza huduma mbali mbali za afya ikiwemo za macho katika jamii ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.

Kwa upande wake Daktari dhamana wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Dkt. Himid Said amesema kumekua na tabia ya baadhi ya wanajamii wanaopewa rufaa katika kambi mbali mbali za matibabu kutokufika sehemu walizoelekezwa kwa ajili ya matibabu zaidi.

Hivyo ameitaka jamii kuzitumia rufaa hizo kwani wizara imeandaa utaratibu nzuri wa kuwapokea wagonjwa hao na matibabu yake yanapatikana bila malipo.

Nae Mratibu wa Christian Blind Mission Zanzibar Mkelemi Abdulrahman amesema taasisi yao itaendelea kushirikiana na serikali katika kutoa huduma mbali mbali kwa jamii ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.

Kwa upande wa wananchi walionufaika na matibabu hayo wamezishukuru taasisi zilizoandaa kambi hiyo na kuwaomba kuendelea kutoa huduma mbali mbali za afya mara kwa mara

Zaidi ya wananchi 200 wamechunguzwa uoni wao na kubainika na matatizo ya uoni hafifu, presha ya macho, macho kuwasha na wamepatiwa matibabu mbali mbali.

Katika hatua nyengine, Mkurugenzi Kinga na Elimu ya afya ametembelea katika kituo cha afya Tumbatu Gomani kwa lengo la kujionea utolewaji wa huduma mbali mbali za afya ikiwemo afya ya mama na mtoto na kuwataka wazazi na walezi kuwapeleka Watoto wao kituoni hapo kupata chanjo.

Loading