Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Itaendelea kudhibiti bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya Mwanaadamu

WIZARA ya Afya Zanzibar kupitia Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi itaendelea kudhibiti bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya mwanadamu ili kuondokana na maradhi mbali mbali yakiwemo yasioyakuambukiza.

Akizundua Bodi ya Pili ya ushauri ya Wakala Chakula, Dawa na Vipodozi ZFDA Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema kupatikana kwa Bodi hiyo kutaengeza ufanisi wa kazi kwa Taasisi hiyo katika masuala mazima ya udhibiti wa bidhaa mbali mbali zinazoingia hapa nchini kwa kuweza kuondokana na maradhi mbali mbali yakiwemo yasiombukiza.

Amefahamisha kuwa Zanzibar kama nnchi nyengine za dunia ya tatu bado inaendelea kwa kiasi kikubwa kutegemea bidhaa nyingi kutoka nchi za nnje ikiwemo Chakula, dawa na Vipodozi, hivyo amekitaka chombo hicho kusimamia vyema bidhaa hizo ili zisiweze kuleta madhara kwa watumiaji.

Amesema kuwepo kwa Bodi hiyo ni sehemu ya utekelezaji na uimarishaji wa utawala bora katika sekta ya afya hapa nchini katika Nyanja za udhibiti wa ubora, ufanisi na usalama wa Bidhaa za Chakula, Dawa na vipodozi pamoja na vifaa tiba na teknolojia mbali mbali za afya.

Aidha alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na vipodozi itaendelea kusimamia na kudhibiti bidhaa hizo ili zisiweze kuleta madhara ya kiafya kwa jamii.

Ameitaka Bodi hiyo kusimamia na kutoa ushauri wa karibu hasa katika kipindi hichi Wizara ya Afya ambacho kina mashirikiano na taasisi binafsi katika kutoa huduma za Afya hapa nchini kufuatia miundo mbinu mipya ya afya zikiwemo Hospitali za Mkoa na Wilaya Unguja na Pemba.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh ameitaka bodi hiyo kufanya kazi kwa bidii na umahiri mkubwa ili lengo la kuimarisha afya za wananchi litimie na kuondoka na maradhi yanayotokana na bidhaa zisizofaa.

Nae Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt Salum Seif Salum amesema katika kuimarisha Bodi hiyo watahakikisha wanasimamia na kuwa waaminifu katika utekelezaji wa kazi zao.

 

Loading