Uwepo wa sera ya Maabara hapa nchini kutasaidia kuimarisha huduma za Afya

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema kuwepo kwa sera ya Maabara hapa nchini kutasaidia kuimarisha huduma za Afya.

Akifungua mkutano wa kupitia Rasimu ya Sera na muongozo wa Maabara kwa viongozi wa Wizara ya Afya, Wakuu wa vitengo pamoja na wadau mbali mbali Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Amour Suleiman Mohamed amesema hatua ya kuwa na sera hiyo kutawezesha utekelezaji katika ngazazi tofauti za utoajia wa huduma.

Amesema Sera ndio muongozo Mkuu wa utoaji wa huduma katika sehemu mbali mbali ikiwemo za kimaabara katika hospitali na vituo vya Afya  na Zanzibar kulikuwa hakuna muongozo wa utoaji wa huduma hizo, hivyo kuwepo kwa sera hiyo kutafanikisha kwa kiasi kikubwa huduma kuwa zenye ubora.

Amefahamisha kuwa kutokana na kukosekana kwa sera ya Maabara kwa kipindi kirefu wafanyakazi wa Maabara kila mmoja alikuwa anafanya kazi zake kwa mujibu anavoona ni sahihi kwa mujibu wa elimu yake na taaluma yake, hivyo baada ya kuwa na muongozo huu ambao unatarajiwa kupitishwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya utasaidia kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Amesema mara baada ya kupitishwa kwa sera hiyo kila Mtaalamu wa Maabara ahakikishe anafanya kazi zake kwa kufuata sera muongozo huo na kuwataka wataalamu hao kuhakikisha kuwa muongozo huo uguse kila eneo la upimaji wa kimaabara.

Kwa upande wake Meneja Miradi kutoka ICAP Dkt Haji Hussein amesema katika kufanikisha Sera hiyo wameshirikiana na Wizara ya Afya kuangalia vipaumbele  vya sera hiyo ili kuweza kutekelezwa katika ngazi ya Maabara.

Amesema kwa sasa tayari wameshatengeneza mingozo mitatu miwili kwa Tanzania bara na mmoja wa Zanzibar, ambayo itahusisha kuwapatia mafunzo wafanyakazi wa maabara pamoja na kusadia wafanyakazi wa maabara kufatilia kila maradhi kupitia maabara yao.

Kwa upande wake Meneja  wa maradhi yasiopewa kipaumbele NTD Dkt Shaali  Ame amesema wanatarajia Sera na Mongozo huo utazingatia masuala mazima maabara zote za hapa nchini.

Mkutano huo wa kupitisha sera na muongozo wa mabara umafanyika kwa mashirikiano ya wizara ya afya Zanzibar ,ICAP na Shirika la CDC Tanzania.

Loading