Wizara ya Afya Zanzibar imesema itafanya jitihada za makusudi kuhakikisha mawasiliano yanafanyika kwa maabara zote za Afya nchini

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema itafanya jitihada za makusudi kuona kuwa mawasiliano yanafanyika kwa maabara za Afya na maabara nyengine hapa nchini kwa lengo la kukabiliana na magonjwa mbali mbali yakiwemo ya miripuko.

Akizungumza katika mkutano wa kupitia Muongozo wa Maabara kwa wadau mbali mbali, Mkurugenzi Tiba wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Marijan Msafiri amesema uthibitisho wa maradhi mengi unafanyika maabara na baadae zoezi zima la kukabiliana maradhi husika linafanyika.

Amesema ni vyema kuwepo kwa mashirikiano ya karibu baina ya maabara za afya na maabara nyengine zikiwemo za wanyama kutokana na kuwa baadhi ya maradhi yanatoka kutoka kwa wanyama kwenda kwa binaadamu, matumizi mabaya ya dawa za antibayotiki ambayo husababisha usugu kwa vimelea vya maradhi hayo.

Amefahamisha kuwa katika kukabiliana na hali ya matumizi ya dawa za antibayotiki Wizara ya Afya inashirikiana kwa karibu na wadau wengine katika kudhibiti matumizi ya dawa hizo kwa kutekeleza mikakati ya usugu wa vijidudu na wanaendelea kufuatilia mwenendo wa maradhi yanapoibuka.

Amewataka wadau hao kuipitia  Muongozo huo na kuweka mikakati ambayo kila mtaalamu wa Maabara kuhakikisha anafanya kazi zake kwa kufuata sera muongozo huo mara baada ya kukamilika kwake.

Dkt Marijani amesema ili kuweza kukabiliana na maradhi mbali mbali Wizara ya Afya itaendela kushirikiana na Wizara Nyengine ili maradhi yanapoibuka kuweza kufanya kazi kwa pamoja na kuweza kuyaondoa mara moja.

Kwa upande wa Mtaalamu wa Afya  kutoka Shirika la CDC Tanzania Saida Murugwa   amesema kuwa kwenye magonjwa ya miripuko hakuna magonjwa ya taasisi moja ni vyema kufanya kazi kwa pamoja kunasaidia kuyaondosha mara moja maradhi yanapoingia katika nchi na kuwepo kwa sera ya maabara itasaidia hali hiyo kutokana na kuwa imehusisha sehemu zote muhimu.

Nae mwakilishi kuto ICAP Dkt Haji Hussein amesema kuwa  Taasisi yao imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuhakikisha kuwa vipaumbele vya Afya vinatimia kwa ufanisi zaidi hasa katika upande wa maabara.

Amesema kukutana kwa wataalamu hao ni njia moja wapo ya kusaidia kutoa utaalamu wao wa kuimarisha muongozo wa wataalamu wa maabara ambao utaenda kusaidia maabara ziweze kuripoti vizuri magonjwa kwa wakati na kuhakikisha yanapatiwa ufumbuzi mapema.

Mkuu wa huduma za uchunguzi wizara ya afya  Zanzibar Abdallah Said Mohamed amesema baada ya kukamilika kwa  muongozo huo kutakua na rasimu ya kwanza ambayo itajadiliwa  kwa kina na wadau wengine ili kuweza kupata mawazo yatakayofanya muongozo huo kuwa wenye ubora zaidi.

Mkutano huo  umeandaliwa na wizara ya afya kwa mashirikiano makubwa na shirika la ICAP na CDC Tanzania.

Loading