Taarifa ya utafiti wa kitaifa wa hali ya lishe kwa skuli za msingi na sekondari Zanzibar

MKUU wa Kitengo cha Lishe Zanzibar Asha Hassan Salmini amesema asilimia 52 ya watoto kuanzia miaka 5-9 waupungufu wa damu.

Hayo aliyaeleza wakati akitoa taarifa ya utafiti  wa kitaifa wa afya lishe katika skuli za msingi na Sekondari wa mwaka 2021/2022 kwa waandishi wa habari huko Kidongochekundu mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema  kwamba upungufu wa damu ni tatizo kubwa ambalo linatokana na na watu kutojichunguza afya zao hasa wakati wakiwa wajawazito ambapo athari yake huwakumba na watoto.

Hivyo alisema kwamba kutokana na hali hiyo waliamuwa kufanya utafiti huo kwa vijana kuanzia miaka 5-19 ili kujua chanzo cha tatizo hilo.

Hata hivyo alisema asilimia 46 ya vijana kuanzia miaka 15-19 wana upungufu wa damu  wakiwemo wanawake na wanaume .

Alifahamisha umri huo wa ujana huambatana na ukuaji wa haraka , ongezeko la damu na utanukaji wa misuli ambayo huongeza mahitaji ya mwili ya maadini chuma ambayo ni muhimu kwa binadamu.

Hivyo alisema folik aside inahitajika kwa utengenezaji  wa haraka na ukuaji wa chembe nyekundu za damu na kusema kwamba matatizo hayo yasiporekebishwa yanaweza kuendelea na kuathiri afya ya lishe hapo baadae.

“Ni muhimu kuvunja mzunguuko huu kwa kuwekeza kwenye lishe bora katika vipindi mbali mbali vya ukuaji ili kumjenga mtoto kukuwa katika afya iliyo bora.

Hata hivyo alisema kwamba ukosefu wa taarifa za afya na lishe kwa watoto kuanzia miaka 5-19 ni taarifa muhimu kwa kuweka mikakati ya kuimarisha afya na lishe kwa watoto.

Aidha alisema kwamba  utafiti huo umebainisha kwamba asilima kubwa ya watoto wanatumia chakula kisicho na ubora unaohitajika.

Utafiti huo ulijumuisha skuli 53 za wilaya 11 za Zanzibar ulikuwa na lengo la kutathmini lishe ikiwemo ulaji, ubora wa chakula kinacholiwa na ubora wa ulaji pamoja na kutathmini mazingira ya afya ya lishe katika skuli ikijumuisha miundombinu, viwanja vya michezo, bustani, kantini, miundombinu ya ulaji, utekelezaji wa mikakati ya afya na lishe ikiwemo ulishaji skuli.

Hata hivyo alielezea kwamba katika utafiti huo waligunduwa kwamba wasichana wengi zaidi ya 46 anatumia chakula kisicho bora ikilinganishwa na wavulana ambao ni asilimia 23, hali inayopelekea kuwa na upungufu wa damu.

Aidha alipendekeza kuimarisha utekelezaji wa program za afya na lishe skuli, ikiwa ni[pamoja na kuhakikisha ulishaji skuli unafikiwa katika skuli nyingi pamoja na kutengeneza kifurushi cha mawasiliano ya mabadiliko ya tabiaya kijamii ya afya na lishe  (SBCC) na kuhamasisha juu ya ulaji na mitindo bora ya maisha.

Hata hivyo alisema kwamba jambo jengine la kufanya ni kuhakikisha uwepo wa mazingira yanayolinda afya kwenye skuli ambayo yanaimarisha ulaji bora na ufanyaji wa mazoezi kupitia uundaji wa miongozo na ufuatiliaji .

Asha alisema kwamba mbali na kufanya tatifiti lakini wamekuwa wakichukuwa hatua mbali mbali ikiwemo maandalizi ya afya lihse skuli, maandalizi ya miongozo ya afya lishe skuli, kujenga uwezo wa waalimu na wahudumu wa afya kwenye kutoa huduma za lishe kwa watoto na vijana baleghe  kwenye skuli za msingi na sekondari.

Loading