Maadhimisho ya wiki ya maabara Duniani

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema, serikali itaendelea kuziimarisha maabara kwa lengo la kupata matokeo sahihi ya vipimo na tafiti za kimaabara nchini.

Dk. Mwinyi, aliyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla katika mkutano wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya maabara duniani, yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni jijini Zanzibar jana.

Alisema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeamua kutenga kiasi kikubwa cha fedha katika kuimarisha maabara kwa kuzipatia mashine na vifaa vya kisasa hali ambayo imesaidia kupunguza kupeleka ‘vinasaba’ kuchunguzwa nje ya nchi.

Dk.Mwinyi, alisema, serikali imeanzisha utaratibu wa kuzishirikisha taasisi na kampuni binafsi katika utoaji wa huduma za maabara za afya katika hospitali kwa lengo la kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za maabara pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji.

Aidha, alieleza, kuanzishwa kwa maadhimisho ya wiki ya maabara Zanzibar, kutapelekea kuwa na jukwaa litakalowaunganisha wataalamu wa maabara ndani na nje ya nchi hatua ambayo itatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na utaalamu katika kufanya vipimo na majaribio mbali mbali ya tafiti.

Aidha, alieleza, kuanzishwa na kuendelezwa maadhimisho ya wiki ya maabara duniani hapa Zanzibar kutasaidia kuimarika kwa vitengo na Jumuiya za Wataalamu wa Maabara za Afya nchini.

Akigusia suala la ajira kwa wataalamu wa maabara, Dk. Mwinyi, alisema, serikali itaendelea kuajiri wataalamu hao kwa mujibu wa mahitaji na kueleza kuwa hospitali zilizopo na zinazoendelea kujengwa zinahitaji wataalamu hao ili wananchi wapate huduma bora, zenye urahisi na haraka.

Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi, alisema, serikali kwa kutambua afya za wananchi wake, imeandaa mpango wa kuziimarisha  huduma za maabara kwenye vituo vya mifugo na uvuvi ili ziweze kutoa nyama, maziwa na samaki wenye usalama kwa afya za binadamu.

Aidha, aliwashauri wataalamu wa maabara za kilimo, mifugo na uvuvi kuandaa mipango mikakati ili kuleta mapendekezo ya kuziimarisha maabara hiz ili kwenda sambamba na dunia inayozungumza mkakati wa sera ya afya moja.

Pamoja na hayo, Dk. Mwinyi, aliwahakikisha wataalamu hao wa maabara kuwa serikali italinda na kusimamia maslahi yao ili kuiendeleza kada hiyo pamoja na kuimarisha mazingira yao ya kazi.

Kwa upande wake, Kaimu Waziri wa Afya, Riziki Pembe Juma ambae ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, alieleza kuwa kada ya maabara ni muhimu kwa kuwa inatoa mchango mkubwa katika kukuza ustawi wa jamii kwa kuwahakikishia usalama wa afya za wananchi.

Aidha, aliwataka wataalamu hao kushirikiana na wataalamu wengine kwa kutumia matokeo ya tafiti za wataalamu hao ili kukuza ustawi wa wananchi.

Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wataalamu wa Maabara Zanzibar (ZAMELSO), Hamad Bakar Magarawa, alieleza,   Zanzibar kwa mara ya kwanza imeungana na nchi nyengine kwa kuadhimisha wiki hiyo ambapo itaweza kusaidia kukuza kada hiyo nchini.

Awali,  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alitembelea mabanda ya maonesho ya kazi za maabara na kujionea juhudi mbali mbali zinazofanywa na wataalamu hao na kusifu hatua zilizofikiwa kupitia kada hiyo.

 

Loading