Utoaji elimu juu ya huduma za maabara inahitajika kwa wananchi

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdulghulam Hussein, amesema, utoaji elimu juu ya matumizi sahihi ya huduma za maabara inahitajika kufikishwa kwa umma ili kujenga taifa lenye afya njema.

Hayo aliyaeleza wakati akifungua maonyesho ya wiki ya maabara duniani huko viwanja vya Muembe Kisonge jana.

Alisema, bado wananchi wengi wanashindwa kufahamu kazi za maabara na kujikuta wakishindwa kupata huduma na shughuli mbalimbali zinazofanywa na wanataaluma wa sayansi za afya.

Hivyo, aliwahimiza wananchi kuitumia kikamilifu wiki ya huduma za maabara ili waelimike na kupata ufumbuzi wa maradhi mbalimbali yanayowanyemelea.

Aidha, alisema, wiki hiyo ya huduma za maabara itakuwa na faida kwa wananchi kwa vile wamepata huduma mbalimbali zikiwemo za kiuchunguzi na ushauri kwa ajili ya afya zao.

Mapema Mkemia Mkuu wa Serikali, Farid Mzee Mpatani, alisema, utoaji wa huduma bora za afya maabara imekua kiungo muhimu kwenye utabumbuzi wa magonjwa, kufuatilia mwenendo na maendeleo ya matibabu ya wagonjwa.

“Maabara ya tiba imekua kitovu cha tafiti za kiafya ambazo zinatoa takwimu za hali ya maambukizi ya magonjwa mbalimbali”.

“Lakini pia takwimu zinazosaidia watunga sera na mamlaka kupanga mikakati ya kiutendaji kwa ushahihi.

Mratibu wa wiki ya maabara, Mwinyi Issa Mselem, alisema, alitoa wito kwa vijana kusomea masomo ya sayansi ili waweze kupata fursa ya kujiajiri na kuajiriwa ikiwemo maabara.

“Vijana wachangamkie masomo hayo kwani bado taifa linawahitaji aina hii ya wataalamu wa huduma za maabara.

Maonyesho hayo ya wiki ya huduma za maabara ambayo huadhimishwa kila mwaka mwishoni mwa Aprili yamefanywa na Baraza la Wataalamu wa Maabara na Jumuiya Wataalamu wa Maabara Zanzibar (ZAMELSO) na kilele chake kitafanyika kesho.

Loading