SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema itaendelea kuimarisha huduma za afya ya msingi kwa maeneo yote ya Unguja na Pemba ikiwa na lengo la kuboresha huduma za uzazi salama, matibabu ya meno na kinywa, uchunguzi wa ‘ultra sound” na huduma za maabara zipatikane kwa ufanisi wenye vituo vya afya vyote vya msingi kwa maeneo yote ya nchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameyasema hayo kwenye ufunguzi wa kituo cha Afya, Bubwini Makoba, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema, Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu, upatikaji wa dawa muhimu, vifaa tiba, na rasilimali watu ikiwemo madaktari, wauguzi, wafamasia na wataalamu wengine muhimu wanaohitajika katika sekta ya afya.
Aidha, Dk. Mwinyi alieleza azma ya Serikali kujenga nyumba za wafanyakazi kwa baadhi ya hospitali za Wilaya, Unguja na Pemba ili kupunguza tatizo la makaazi kwa watumishi wa sekta ya afya na kuwafanya wabakie kwenye vituo vyao vya kazi muda wote ili waendee kutoa huduma hasa kwa kesi za dharura.
Alieleza, hatua hiyo itaboresha zaidi mfumo wa rufaa na kupunguza kwa kiasi kikubwa kasi ya wagonjwa kwenda Hospitali ya Mnazi Mmoja na kupunguza mrundikano wa wagonjwa Mnazi mmoja.
Dk. Mwinyi alisema, licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto kwenye sekta ya Afya zikiwemo uhaba wa wafanyakazi mabingwa na wabobezi kwenye kada mbali mbali za Afya, hali aliyoielezea inaisababishia Serikali kutumia fedha nyingi kwa matibabu ya wananchi nje ya Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi, alieleza katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imeamua kushirikiana na sekta binafsi ambao wataendelea kuhudumia hospitali za Serikali zikiwemo huduma za uchunguzi wa maradhi hasa kwa maeneo yaliyoimarika kwenye utekelezaji wake.
Alisema nia ya Serikali ni kufikia malengo iliyojipangia ya kuwahikishia wananchi wake huduma nzuri ndani ya wakati unaotakiwa kwenye hospitali na vituo vyote vya Afya vya maeneo yote nchini.
“Nimeamua kulieleza hili kwa vile kuna baadhi ya watu kwa makusudi wameanza kupotosha na kuwadanganya wananchi, utaratibu huu umeanza kutumika kwa mafanikio katika hospitali ya Mnazi Mmoja na utaendelezwa kwenye hospitali zetu zote za Wilaya pamoja na hospitali ya Mkoa ya Lumumba iliopo Mkoa wa Mjini Magharibi” Alibainisha Dk. Mwinyi.
Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi aliwaagiza watumishi wote watakapelekwa kufanya kazi kituo cha Afya Bumbwini Makoba wajitahidi kuitunza miundombinu iliyopo, kufanyakazi kwa moyo wa kujitolea na huruma kwa wagonjwa na kuzingatia maadili ya kazi zao na kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa watakaowahudumia.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Afya, Nassor Ahmeid Mazrui alisema, ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuimarisha vituo vya Afya vya msingi nchi nzima ili kuboresha huduma za Afya sambamba na ujenzi wa hospitali 11 zikiwemo 10 za Wilaya na moja ya Mkoa.
Naye, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Amour Suleiman, alisema Ujenzi wa kituo hicho ulianza May 14 mwaka 2022 na kukamilika mwezi June mwaka huu ambao umegharimu shilingi milioni 450, 770, 400 hadi kukamilika kwake ambapo huduma za kliniki mbalimbali zinatolewa na kituo hicho ikiwemo huduma za mama wajawazito na watoto, maabara na ultrasound, vifaa tiba, meno, uangalizi maalum, mashine za kisasa za kupimiamagonjwa yasiyoambukiza ikiwemo presha, sukari na mashine za kupimia umeme wa moyo.