Wakunga na wauguzi waaswa kufanya kazi kwa uweledi kuepuka lawama kutoka kwa wananchi

WAUGUZI na Wakunga nchini wametakiwa kubadilika katika utendaji wa kazi zao   na kuweza kutoa huduma zenye ubora na kundokana na malalamiko kwa wananchi.

Wito huo umetolewa Mkurugenzi Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Zanzibar Mwanaisha Juma Fakih katika kikao cha 29 cha Baraza la Wauguzi na wakunga pamoja na hafla ya kumuaga Mwenyekiti wa Baraza hilo na kumkaribisha Mwenyekiti mpya.

Amesema licha ya juhudu kubwa zinazofanywa na wajumbe wa  Baraza la Uuguzi na  Ukunga ya kuwafaatilia wauguzi na wakunga katika Sehemu zao za kazi pamoja na vyuo vinavyotoa taaluma ya fani hiyo bado kunahitajika jitihada za makusudi kuona kuwa kazi zinafanyika kwa ufanisi mkubwa.

Amefahamisha kuwa katika utekelezaji wa kazi zao katika kada ya Uuguzi na Ukunga watazingatia suala zima la taaluma kwa wafanyakazi wake pamoja na taaluma inayotolewa vyuoni ili kuweza kwenda na wakati juu ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Amelitaka Baraza la Wauguzi na Ukunga kufanya kazi kwa mashirikiano na kuweza kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wafanyakazi na kuwa na usimamizi kwa watoa huduma ili kuweza kuondokana na malalamiko.

Kwa upande wake Mkurugenzi Huduma za Hospitali Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Msafiri Marijani amesema ipo haja ya kuangalia suala zima la taaluma kwa wafanyakazi wake pamoja na wanafunzi waliokuwepo vyuoni ili kuondokana na wafanyakzi ambao hawana ujuzi.

Amesema wafanyakzi wakiwa na ujuzi wa kutosha na kupata stahiki zao na kuwa na usimamizi mzuri kutoka kwa wakuu wao wa kazi pamoja na Baraza wa Wauguzi na Wakunga kutaondokana na malalamiko kwa ndugu wa jamaa za Wagonjwa.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga ambae amemaliza muda wake katika Baraza hilo Amina Abdulkadir amesema bado kada ya Uguuzi na Ukunga inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, lugha chafu kwa wagonjwa na jamaa za wagonjwa, majengo ya kutolea taaluma ya kada hiyo pamoja na ofisi za Baraza hilo.

Amefahamisha kuwa katika kukabiliana na vifo vitokanvyo na uzazi wauguzi na wakunga kuna haja ya kufanya tafiti hasa wanapokuwa sehemu zao za kazi.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la Uguuzi na Ukunga Zanzibar Sharifa Awadh Salmin amesema kuwa atafanya kazi kwa mashirikiano na Baraza hilo kwa lengo la kuimarisha huduma za Afya hapa nchini.

Amesema Wauguzi na Wakunga wanafanya kazi kubwa katika kuwapatia huduma wagonjwa katika hospitali na vituo vya Afya hivyo atahakikisha changamoto zinazowakabili wanazipatia ufumbuzi kwa mashirikiano na Baraza hilo.

Loading