RAIS wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali inawatambua rasmi, wahudumu wa afya ya jamii (CHW) kama wafanyakazi wa afya ya jamii

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali inawatambua rasmi, imewapokea kwa mikono miwili na itawaendekeza kwa kuwakuza katika fani hiyo mpya ya “Community Health Workers” wahudumu wa afya ya jamii kama wafanyakazi wa afya ya jamii .

Dk. Mwinyi alieleza hayo wakati akizindua program hiyo ya kitaifa ya wahudumu wa Afya wa kujitolea Zanzibar katika viwanja vya Maisara Suleiman.

Alisema serikali imeridhia kutelekezwa mpango huo kwa kuzingatia kazi nzuri wanayoifanya, nidhamu yao na faida ya huduma wanazozifanya katika kuimarisha afya za wananchi na kuwatambua rasmi kutoka CHV kuwa CHW.

Aidha alisema uzinduzi wa programu hiyo ni ishara ya matumaini ya wananchi kupata huduma zilizo bora zaidi baada ya kuzinduliwa rasmi.

Dk. Mwinyi alibainisha kuwa kutokana na uzinduzi wa programu hiyo hivi sasa nchi inakuwa ya mwanzo duniani kuweza kusimamisha mpango wa Kitaifa wa Wahudumu wa Afya wa ngazi ya jamii wanaotumia mfumo wa kidigitali.

1Alisema ni dhahiri kuwa kupitia program hii, Zanzibar inapiga hatua nyengine muhimu ya maendeleo ya sekta ya afya kwani kunawezesha kuunganisha huduma za afya nje ya vituo vya afya katika sehemu wanazoishi wananchi.

Alifahamisha kuwa hiyo ni hatua kubwa ya maendeleo katika uimarishaji wa huduma za afya ya jamii ambayo wanajivunia na kutoa fursa kwa mataifa mengine kuja Zanzibar kwa ajili ya kujifunza.

Rais Mwinyi aliwapongeze wahudumu hao kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya katika kuihudumia jamii kwa lengo la kuimarisha afya zao.

Alisema wahudumu hao wanafanya kazi kubwa tokea chini kwenye jamii kwa kupita nyumba hadi nyumba kupata taarifa zinazowasaidia kuweza kutoa huduma kwa ufanisi na kutumia teknolojia ya kisasa ya kidigitali.

Alisema hatua ni muhimu kwani inawajengea uwezo na kuwapa nguvu ya maendeleo hususan katika mifumo ya utoaji wa huduma za afya hapa nchini.

“Naamini tukiendeleza huduma hizi katika ngazi ya jamii kwa wananchi katika ngazi ya jamii basi tutaweza kufanikiwa sana katika utoaji wa huduma za afya kwani hili ndio eneo la kwanza la utoaji huduma ni lazima kuweka nguvu kubwa hapa na kwengine katika eneo la kati na juu,” alisema.

Aliwapingeza kuwapongeza Wahudumu wa afya ya jamii kwa namna wanavyojitoa na kufanya kazi kwa mapenzi na uzalendo mkubwa katika kuihudumia jamii.

Akizujgumzia kaulimbiu ya “Twende pamoja kusaidia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuelekea upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote” alisema kauli mbiu hiyo inabainisha ukweli kazi wanayoifanya wahudumu wa afya ya jamii.

Alisema hawawezi kufanikiwa bila ya kupata usaidizi kutoka kwa jamii yenyewe na wadau wengine kutokana na ugumu wa kazi yenyewe.

Hivyo, aliishauri jamii kuwasaidia watu hao na kuwapa ushirikiano wa kutosha ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao.
Akizungumzia changamoto za wahudumu hao ikiwemo kupatiwa posho ndongo ya 47,000 alisema katika utaratibu huo mpya posho hiyo itakuwa mara tatu zaidi ya hiyo, kupatiwa simu mpya 3000 zilizotolewa na Tigo Zanztel na kuiagiza wizara ya afya kuondoa tatizo la kuchelewesha malipo wakati wa mafunzo.

Aliwahakikishia kwamba serikali itaendelea kuchukua hatua za kuimarisha sekta ya afya kwa kuimarisha miundombinu na kuwepo kwa vifaa vya kisasa vya utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Tutahakikisha huduma hizi zinawafikia wananchi wote kuanzia katika huduma za ngazi ya jamii kwenye msingi hadi katika ngazi ya rufaa,” alisema.

Rais Mwinyi aliwahakikishia wahisani kuwa serikali inathamini sana mchango wao katika jitihada za kuimarisha huduma za afya nchini na kutoa kila aina ya ushirikiano katika kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwa program hiyo yanafikiwa.

Aliahidi kwamba serikali kupitia Wizara ya Afya, itahakikisha program hiyo inaendelea hata baada ya wahisani na Wafadhili hao kuacha mkono kutokana na umuhimu wake.

Naye Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, alisema wahudumu hao ni kiungo muhimu cha wizara katika ngazi ya jamii kwani wanafanya kazi kubwa ya kuisaidia serikali katika kutoa elimu na huduma za afya kwa wananchi.

Alisema wizara ya afya inajibunia kupata kiungo madhubuti katika ngazi ya jamii ili kutoa huduma za jamii na kuwatambua wahudumu hao ili kuongeza ufanisi katika kazi zao na kuwatambulisha rasmi katika jamii.

Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Amour Suleiman Mohammed wahudumu hao wamekuwa wakitoa huduma katika ngazi ya jamii ikiwemo kutoa elimu ya afya juu magojwa mbalimbali hasa kwenye eneo la mama na mtoto, kusaidia rufaa kwa wanajamii wenye matatizo ya kiafya au viashiria vya hatari dhidi ya magonjwa mbalimbali na kuwaunganisha katika vituo vya Afya kwa matibabu sahihi na kwa wakati.

Alisema wahudumu hao wamekuwa wakiibua matatizo ya kiafya na kuyaripoti katika taasisi husika, kuibua watoto walioasi chanjo, waliokuwa hawajapata chanjo hata mara moja na kuwaunganisha katika vituo vya Afya na kupatiwa chanjo.

Hata hivyo alifahamisha kuwa pia wanailinda jamii juu ya magonjwa ya miripuko yatokanayo na magonjwa yanayodhibitiwa kwa chanjo na kushiriki katika kampeni zote za kiafya kwenye shehia zao, ugawaji wa vifaa mbalimbali vya kiafya kwenye jamii kama vile vyandarua, ugawaji wa dawa za minyoo na matende na mengine yanayofanana na hayo.

Sambamba na hayo alisema pia huduma nyengine kukusanya taarifa za kiafya au zenye muelekeo wa afya kupitia tafiti mbalimbali ili kusaidia mabadiliko ya mipango ya kiutendaji, kusaidia mapambano dhidi udhibiti na kinga juu ya magonjwa ya miripuko.

Alisema Zanzibar ndio ya mwanzo kusimamisha wahudumu wa afya ambapo kupitia program hiyo wameweza kusajili wanajamii asilimia 85 na kupunguza wimbi la wajawazito kujifungulia majumbani na kupunguza vifo vya mama na watoto, vifo vya utapia mlo na maradhi mengine.

Nao wadau wa Maendeleo wakiwemo UNICEF, D- Tree na USAID walisema wataendeleza ushirikiano uliopo baina ya mashirika yao na serikali katika kuendeleza huduma za afya na maendeleo kwa ujumla.

Sambamba na hayo waliipongeza serikali kuwatambua vijana hao kwani ni njia moja ya kuibua huduma za awali za afya katika ngazi ya jamii

Akisoma risala kwa niaba ya wahudumu wenzake 2300 Unguja na Pemba, Ali Yahya Rashid,alisema tokea walipoanza kazi mwaka 2020 waliapatiwa Elimu ya Afya na mazingira ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi

Alisema pamoja na mafanikio mbalimbali lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo posho ndogo wanayopokea kwa mwezi, kuchakaa kwa simu kutokana na utendaji kazi zao, kukosa sare na vitambulisho.

Loading