Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi anatarajiwa kuzindua Programu ya Kitaifa ya Wahudumu wa Afya wa Kujitolea Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuzindua program ya kitaifa ya wahudumu wa afya wa kujitolea ili kutilia mkazo katika kuwatambua rasmi, kuwajengea uwezo kitaalamu na kuwawekea mazingira wezeshi ya utendaji kazi.

Akitoa taarifa jana kwa waandishi wa habari huko katika ofisi za Wizara ya Afya Mnazimmoja, Waziri wa Wizara hiyo Nassor Ahmed Mazrui, alisema wanataka kuwatambulisha rasmi wahudumu hao kama ni kiungo muhimu cha wizara katika ngazi ya jamii.

Alisema, lengo hilo ni kuongeza uelewa kwa wazanzibari wote na wadau wa maendeleo kuwatambua wahudumu wa Afya wa ngazi ya jamii ili wawape ushirikiano zaidi pamoja na misaada inyostahili ili kuongeza ufanisi wa kazi zao.

“Tunataka kuishawishi serikali pamoja na wadau mbalimbali kuelekeza vipaumbele vyao kwenye mstakbala huu mwema, ili watenge fedha za kusaidia utekelezaji wa mipango ya afya ya jamii ikiwemo kuwawekea mazingira wezeshi ya utendaji wa kazi zao,” alisema.

Aidha alisema, wanakusudia kuwahabarisha wananchi na wadau mbalimbali juu ya azma ya wizara ya Afya katika
mabadiliko yanatarajiwa hivi karibuni kwa wahudumu hao ni kuifanya kuwa kada rasmi inayotambulika na kukubalika katika wizara ya Afya.

Waziri Mazrui alibainisha pia lengo jengine ni kuifanya kuwa kada ya kitaaluma, na taratibu kuweza kuiunganisha kada hiyo kwenye mfumo wa ajira kadiri ya hali itakaporuhusu na kuongeza idadi ya wahudumu hao kutoka 2300 waliokuwepo sasa wanaohudumia Shehia za Zanzibar na kufikia 3000 ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuokoa vifo vinavyozuilika Zanzibar.

Hata hivyo alisema wizara inataka kupandisha posho lao la mwezi kulingana na kazi zao kadiri hali itakaporuhusu, kujengewa uwezo kwa kupatiwa mafunzo ya muda mrefu ya kinadharia na kivitendo ili waweze kufanya kazi kwa ufasaha na ufanisi wa hali ya juu.

“Mipango hii yote itaweza kutekelezeka vyema ikiwa tu tutaweza kuungana pamoja na kusaidia kupeleka mbele azma hii,” alisema

Sambamba na hayo Waziri Mazrui alisema, Wizara ya Afya Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, mashirika na taasisi mbalimbali wapo katika mapambano makubwa ya kuimarisha afya za wazanzibari kupitia mpango wa kitaifa wa wahudumu wa Afya wa ngazi ya jamii Zanzibar.

Alisema, Programu hiyo ya kitaifa ya wahudumu wa Afya ngazi ya jamii visiwani Zanzibar ilianza rasmi mwaka 2018-2019.

Alisema, huduma hizo ni pamoja na kutoa elimu ya afya juu magojwa mbalimbali hasa kwenye eneo la mama na mtoto, kusaidia rufaa kwa wanajamii wenye matatizo ya kiafya au viashiria vya hatari dhidi ya magonjwa mbalimbali na kuwaunganisha katika vituo vya Afya kwa matibabu sahihi nakwa wakati muafaka.

Huduma nyengine alisema ni pamoja na kuibua matatizo ya kiafya na kuyaripoti katika taasisi husika, kuibua watoto walioasi chanjo, waliokuwa hawajapata chanjo hata mara moja na kuwaunganisha katika vituo vya Afya kupatiwa chanjo ili waimarishe afya zao na kuilinda jamii juu ya magonjwa ya miripuko yatokanayo na magonjwa yanayodhibitiwa kwa chanjo.

Lakini pia kushiriki katika kampeni zote za kiafya kwenye shehia zao, ugawaji wa vifaa mbalimbali vya kiafya kwenye jamii kama vile vyandarua, ugawaji wa
dawa za minyoo na matende na mengine yanayofanana na hayo.

Sambamba na hayo alisema pia huduma nyengine kukusanya taarifa za kiafya au zenye muelekeo wa afya kupitia tafiti mbalimbali ili kusaidia mabadiliko ya mipango ya kiutendaji, kusaidia mapambano dhidi udhibiti na kinga juu ya magonjwa ya miripuko.

Alibainisha kuwa Wizara ya Afya imeshuhudia mafanikio na maendeleo makubwa ya kiafya kwa wanajamii kupitia program hiy hasa katika kufikia dhamira ya Shirika la Afya duniani ya upatikanaji wa afya kwa wote.

“Zanzibar ni nchi ya mwanzo kwa Afrika mashariki na kwengineko duniani kuweza kusimamisha mpango wa kitaifa wa wahudumu wa Afya wa ngazi ya jamii wanaotumia mfumo wa kidijitali ambao wanafanya kazi kwa kutekeleza vipaumbele vya serikali na mipango ya nchi,” alisema

Hivyo, alibaimisha kuwa wanakila sababu ya kujivunia mafanikio hayo ili na wengine waige mfano huo mzuri.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza wadau wa Maendeleo ikiwemo Shirika la D- Tree Tanzania na UNICEF kwa kuunga mkono wahudumu hao wa Afya ya Jamii kwa kuwapatia Mafunzo na Elimu kuona wanatekeleza kazi zao vizuri.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika tarehe 16 Disemba 16 mwaka huu katika viwanja vya Maisara ambapo kauli mbiu yake ni ‘Twende pamoja kuwaunga mkono wahudumu wa afya ya jamii, kuelekea afya kwa wote’.

Loading