Naibu Waziri wa Afya Amesema Serikali Inawatambua Rasmi Wahudumu wa Afya wa Jamii (CHW)

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kuwatambua wafanyakazi wa afya ya jamii (CHW) kwa vitendo.

Ameyasema hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na stahiki za malipo kwa wafanyakazi hao,huko Ofisi za Wizara hiyo Mnazimmoja Mjini Unguja.

Alieleza kuwa taratibu zote za kazi na malipo kwa wafanyakazi hao zinaendelea kufanyiwa kazi na Wizara ya Afya kupitia Idara ya kinga baada ya kurasimishwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi kutoka wahudumu wa Afya wa kujitolea (CHV) kuwa wafanyakazi wa Afya ya jamii (CHW) Disemba 16 mwaka jana.

“kuanzia mwezi Januari ,2024 stahiki za wafanyakazi wetu hawa zitatoka wizara ya afya kupitia idara yetu ya kinga”.alifafanua Naibu Waziri

Aidha alisema kwa kutambua na kuthamini mchango unaotolewa na wafanyakazi hao katika kutoa huduma za Afya kwa jamii Wizara imejipanga kuwaboresha wafanyakazi hao kwa kuwapatia mafunzo ya miezi 6 yatakayoambatana na mitihani ili kuimarisha utendaji wao .

Zaidi ya wafanyakazi 2000 wamerasimishwa kutoka wahudumu wa Afya ya jamii wa kujitolea (CHV) na kuwa wafanyakazi wa Afya katika ngazi ya jamii ( CHW), ambapo awali walikua wakipata stahiki zao kupitia Taasisi ya D-tree.

Loading