WIZARA ya Afya Zanzibar imeripoti kuwa na idadi ya wagonjwa wa Malaria 5,300 mwaka huu wa 2024 walioripotiwa katika vituo vya afya na hospitali ambapo kisiwa cha Unguja kilikuwa na wagonjwa 5020 na Pemba 280.
Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari Afisa wa Afya ya Jamii Wizara ya afya Programu ya kumaliza Malaria Zanzibar Mwinyi Khamis amesema kati ya wagonjwa hao wa malaria walioripotiwa 11 walifariki dunia kutoka Januari mosi hadi Januari 26.
Alisema kwa mwaka 2023 idadi ya wagonjwa walikuwa 18,174 kwa Zanzibar nzima ambapo Unguja ni 17,567 na Pemba 607, wanaume wanaongoza kwa kupata ugonjwa huo, huku waendesha bodaboda wakiwa ni wengi waliopata malaria kutokana na mazingira wanayokaa katika biashara hiyo.
Alisema wanaume wengi wamepata malaria kwa sababu ya kukaa nje muda mrefu hasa nyakati za usiku na kushambuliwa na Mbu wa malaria ikilinganishwa na wanawake.
“Asilimia 66.7 ni wanaume waliopata malaria ikilinganishwa na wanawake ambao walikuwa asilimia 33.3 na wagonjwa 334 walilazwa hospitali kwa kupatiwa matibabu”alisema Afisa huyo.
Aidha alisema wilaya zote Unguja na Pemba zimeathiriwa na ugonjwa huo ambapo wilaya ya Mjini Unguja inaongoza na makundi yalioathirika ni waendesha bodaboda, mafunzi ujenzi hasa wanaojenga nyakati za usiku, wanaokwenda kumbi za starehe na watazamaji wa mpira nyakati za usiku na umri ulioathirika ni miaka 15 hadi 45.
Alisema mambo yaliopelekea kurudi kwa kasi kwa ugonjwa wa malaria Zanzibar ni mabadiliko ya tabia nchi, ikiwemo mvua ambazo hupelekea kutengeneza mazalia ya mbu kutokana na kutuwama kwa maji katika baadhi ya sehemu.
Alisema sababu zingine ni mienendo ya watu kusafiri baina ya Zanzibar na Tanzania bara, baadhi ya wanajamii kutotumia afua za kujikinga na malariai kiwemo matumizi ya vyandarua wakati wa kulala, kuchelewa kufika vituo vya afya kwa wenye dalili ya malaria, kutokubadilisha tabia na kutomaliza dozi ya malaria kwa wagonjwa wanaopatiwa matibabu.
Akizunguma kuhusu maradhi ya miripuko, Meneja wa Kitengo cha Elimu ya afya Wizara ya Afya Zanzibar Bakari Hamad Magarawa, amesemama uchafu wa mazingira ni moja ya chanzo cha kuongezeka kwa magonjwa hao ikiwemo majaa ya taka yaliosheheni katika maeneo mbali mbali hapa nchini bila ya kuhifadhiwa.
“Maradhi mengi ya mripuko yanaibuka kwa sababu ya uchafu, bado waandishi wa habari tunahitaji kutumia kalamu zenu vizuri katika kutoa elimu”alisema Magarawa.
Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa Uviko-19 Magarawa alisema ugonjwa bado upo na kwa kuwa Zanzibar ni nchi ya kitalii bado kuna maingiliano na wageni na wagonjwa wanaopatikana kwa sasa ni wale waliochanja chanjo ya ugonjwa huo.
Alisema watu 483,940 wamepatiwa chanjo Zanzibar hadi Disemba 2023 ambao walipatiwa dozi ya mwanzo bila ya kupata chanjo ya nyongeza (kubusti) ambapo wanaume ni asilimia 40 na wanawake asilimia 59 ya waliochanja chanjo ya awali.
“Chanjo ya Uviko -19 inashuka nguvu ya uhalisia ya kukulinda kutoka miezi sita hadi mwaka mmoja na badala ya hapo kama hujapata chanjo ya ziada ugonjwa unaweza kukupata”alisema.
Alisema kila mwezi Zanzibar inawagonjwa wapya wa ugonjwa huo wa Uviko-19 ambapo kwa mwezi wa Disemba mwaka jana wagonjwa 25 waliripotiwa na Januari mwaka huu zaidi ya wagonjwa 10 hivyo aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ikiwemo kuchanja chanjo ya ziada kwa wale ambao walichanja chanjo ya awali na wale ambao hawajachanja kabisa kuchanja.
Katika hatua nyengine akiwasilisha ripoti ya ugonjwa wa macho mekundu Mratibu wa huduma za afya ya msingi ya macho kutoka Wizara ya afya Zanzibar Dkt Rajab Mohamed Hilali amesema jumla ya wagonjwa 12,860 wamepata matibabu ya maradhi ya macho mekundu katika hospitali na vituo vya afya mbali mbali.
Amesema watu saba watano Unguja na wawili Pemba wamepata upofu wa macho kutokana na kutofata ushauri wa kitabibu katika kukabiliana na ugonjwa wa macho mekundu.
Amewataka wananchi kufika hospitalini na vituo vya afya kutibiwa maradhi hayo na kuacha kutumia dawa kila dawa wanayoshauriwa na watu wasiokuwa na taaluma na kitabibu na kuosha macho kwa maji safi bila ya kuongeza kitu chochote ikiwemo chumvi.