Maadhimisho siku ya Maabara Duniani

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wataalamu wa Maabara kuvifanyia utafiti vitu wanavyovichunguza ikiwemo maradhi ili kuyadhibiti kwa njia za kisayansi.

Akisoma hotuba ya rais Mwinyi katika kilele cha wiki ya Maabara Duniani huko Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege Zanzibar, Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui, alisema, kufanya hivyo kutasaidia taasisi kudhibiti maradhi na kuzielekeza njia zinazoshauriwa kirahisi kutokana na kuwepo na ushahidi wa kisayansi.

Aidha, aliwataka wataalamu hao kuongeza nguvu kwenye Taasisi za Tafiti ikiwemo za Taasisi ya Afya ya Binaadamu (ZAHRI), Utafiti wa Mifugo (ZALIRI), Taasisi ya Utafiti wa Safayansi ya Baharini (ZAFIRI) ili kufikia malengo yaliokusudiwa.

Alifahamisha, Maabara zote zina mchango mkubwa kwa maendeleo mbali mbali ikiwemo ya afya na huduma zinazotolewa kwa wananchi, hivyo, serikali itaendelea kuimarisha Maabara zote ili kuweza kuendeleza kazi za uchunguzi wa maradhi, vinasaba, kemikali, pamoja na vyakula.

Akizungumzia Sera ya Maabara Zanzibar, alisema, ni jambo zuri kwani utekelezaji wa kazi za vipimo hasa zinapokuwa zinatekelezwa na wadau tofauti ni vyema kuwepo na miongozo itakayosaidia kulinda mipaka ya kiutendaji, ubora na viwango vinavyojali maslahi mapana ya wanaotegemea huduma kwenye taasisi hizo.

Aidha, aliwasisitiza kushirikiana na kufanya kazi na viongozi pamoja na mashirika ya kimataifa yanayoshughulikia maendeleo kwa lengo la kuleta maendeleo ya kweli kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Hata hivyo, aliwataka wataalamu hao kufanya mapitio ya mipango kazi yao kila robo ya mwaka, miezi sita na mwaka ili kuweza kujifanyia tathmini ya mafanikio na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Tusisubiri mpaka wiki ya maadhimisho ya maabara ndio mkaanza kufanya kazi hivyo hatutaweza kufikia malengo. Serikali inakuaminini na inakutegemeeni kupata mambo mazuri kutoka kwetu”.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Amour Suleiman, alisema, lengo la maadhimisho ya wataalamu wa maabara Zanzibar ni kuungana na wataalamu wengine Duniani na kuona umuhimu wa kazi za Ki –Maabara katika kutoa huduma kwa jamii.

Alisema, dunia huadhimisha siku hiyo kwa Wataalamu wa Maabara za Afya pekee, lakini, kwa upande wa Zanzibar sekta tofauti zimeshiriki kuadhimisha wiki hiyo ikiwemo maabara za Afya, Kilimo, Mifugo, Maji (ZAWA), ZBS, ZFDA,MKEMIA MKUU na ZURA ili kuweka nadharia ya Afya mjumuisho.

Wakitoa salamu za wadau wa maendeleo Mkururugenzi mkaazi wa Shirika la ICAP nchini Tanzania Haruka Maruyama na Wangeci Gatei wa CDC Tanzanzia walisema kupitia Maabara zilizojengwa na kuwa na miumdombinu imara Zanzibar sasa inaweza kujiamini na kuwa na uhakika wa kukabiliana na tishio lolote la miripuko na kulinda afya za wazanzibar wakati yanapotokezea.

Aidha, wameahidi kuendelea kufanyakazi na serikali kupitia Wizara ya Afya ambapo Wizara hiyo imeandaa muongozo wa uwendeshaji wa ufuatiliaji wa maabara, utakaoweza kuimarisha na kugundua mapema magonjwa.

Nao wataalamu wa maabara walisema mbali na mafanikio hayo yanayoonekana katika sekta hiyo bado wataalamu wa Maabara wa Zanzibar hawajaweza kuitumia ipasavyo fursa iliyotangazwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuingia ubia wa uendeshaji wa Maabara za hospitali zilizopo nchini.

“Bado Uendeshaji wa Maabara hizo sio rafiki kwa wahudumu ambao tayari wapo kwenye mfumo rasmi wa ajira wa serikali au wanaotegemewa kuingia kwenye mfumo na wabia waliomo kwenye uendeshaji wa Maabara hizo”.

“Kwa sasa bado hawajatambua kikamilifu umuhimu wa kutumia Wataalamu wa Maabara wa ngazi ya katikati na ile ya wabobezi”, walisema.

Aidha, walisema, kada hiyo inakabiliwa na ukosefu wa waatalamu wahandisi wa vifaa tiba na kuzifanyia matengenezo ya tahadhari mashine hizo pale zinapoharibika na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi na kusabaisha hasara kwani zinanunuliwa kwa gharama kubwa.

Pia, walisema, ukosefu wa waatalamu wa Maabara katika Skuli za Sekondari (Laboratory Technicians) kunapelekea kukosekana kwa usimamizi mzuri wa Maabara na kupelekea baadhi ya vifaa kuharibika kwa haraka.
Awali, walimshukuru Dk. Mwinyi juu ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta za maabara katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake ambapo huduma za uchunguzi zimeimarika , pamoja na kupatikana kwa ajira za wataalamu wa kada hiyo na kada nyengine za afya.

Wamelibainisha kuwa Maabara za kisasa zimejengwa katika hospitali zote 11 za wilaya Unguja na Pemba pamoja na ZFDA kufungwa mashine za kisasa ikiwemo ya HPLC.

Wiki ya maabara huadhimishwa kuanzia Aprili 14 hadi 21 dunia kote ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema maabara ni kila kitu.

Loading