Wizara ya Afya Zanzibar, inatarajia kuanza awamu ya pili ya zoezi la utoaji wa huduma jumuishi ikiwemo chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wote wenye umri wa miaka 14.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya kutoka Wizara ya Afya Zanzibar Ofsini kwake Mnazimmoja Dk. Salim Slim alisema zoezi hilo litaanza Disemba 1 hadi 2 mwaka huu kwa wasichana wote wa Unguja na Pemba.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya ilizindua rasmi chanjo dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi April 19 mwaka 2018 ikiwa ni zaidi ya miaka mitano sasa ili maradhi hayo yasiwe tena tishio kwa wanawake na wasichana hapa Zanzibar.
Alisema zoezi la utoaji wa huduma jumuishi za upimaji wa macho,kuangallia hali ya lishe na utoaji wa chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa awamu ya kwanza lilifanyika Mwezi Juni mwaka huu wa 2023 kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 ambapo vigori 100 walifikiwa katika zoezi hilo.
Aidha, huduma nyengine jumuishi ( za upimaji macho na lishe ) walipatiwa pia watoto wengine wenye umri wa miaka miaka tisa hadi 14 wakiwemo wavulana.
Aidha alisema Saratani ya Mlango wa Kizazi (Cervical Cancer) ndio saratani inayoongoza kwa kuathiri akina mama wengi hapa Tanzania kwani akina mama Zaidi ya 7,000 wanagundulika kuwa na saratani ya mlango wa kizazi kila mwaka.
Mkurugenzi Salim alibainisha kuwa akina mama kati ya 4000 hadi 5000 hufariki kila mwaka Tanzania kutokana na saratani ya mlango wa kizazi (Zaidi ya asilimia 50 hupoteza Maisha).
Alisema hiyo ni idadi kubwa sana ya akina mama wanaopoteza maisha yao kwa ugonjwa huo ambao sasa umepatiwa kinga.
Alisema saratani ya mlango wa kizazi ina athari kubwa kwa akina mama kote ulimwenguni.
Hata hivyo, alisema inakadiriwa kuwa, wastani wa wanawake 528,000 wanagundulika kuwa na Saratani ya mlango wa kizazi kila mwaka na wengi wa wanaoathirika wanatokea katika nchi zinazoendelea ikiwemo Zanzibar ma maradhi hayo ni tatizo kubwa la kiafya kwa Zanzibar.
“Hali hii inatishia ustawi wa akina mama wa Zanzibar na iwapo hatua za kukinga na kudhibiti ugonjwa huu hazikuchukuliwa haraka na kwa umakini, akina mama wengi wataendelea kupoteza maisha kila siku kwa sababu ya ugojnwa wa saratani ya mlango wa kizazi ambao unaweza kuzuilika kwa Chanjo,” alisema.
Akizungumzia njia kubwa tatu za kuthibiti ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi alisema kinga ya awali ni kuhakikisha wasichana wanapata chanjo ya kuwakinga na saratani ya mlango wa kizazi inayojulikana kwa jina la (HPV-Human Papilloma Virus Vaccination).
Alisema chanjo ya HPV inasaidia kinga dhidi ya virusi vya HPV vinavyosababisha saratani ya mlango wa kizazi.
Aidha, Mkurugenzi Salim aliwasisitiza vijana kujiepusha sana na vitendo vya ngono katika umri mdogo, kuepuka uvutaji wa sigara na matumizi ya tumbaku, kuepuka kubeba mimba katika umri mdogo,na baadae kua waaminifu katika ndoa kwa vile virusi vya HPV husambaa Zaidi kwa njia ya kujamiiana.
Mbali na hayo, aliwashauri kinamama wote waliofikia umri wa kuanzia miaka 30 na kuendelea kuenda hospitali au vituo vya Afya kwa kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kubaini kama wana dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi na kupata matibabu stahiki mapema.
Alibainisha kuwa mara nyingi wagonjwa wanaofika kwa ajili ya kupatiwa matibabu wengi wao wanakuwa na saratani ya steji ya mwisho.
Dk. Slim alisema chanjo ya HPV ni kinga dhidi ya virusi vya HPV vinavyosababisha saratani ya mlango wa kizazi.
Alibainisha kwamba chanjo hiyo inazuia wanawake kutoambukizwa virusi vya HPV na hivyo kuwakinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.
Alisema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa chanjo hii inaleta matokeo chanya pale inapotolewa katika umri wa miaka 9 hadi 14 kwa zaidi ya asilimia 95% kwa walengwa.
Alifahamisha kuwa chanjo hii kwa sasa inatolewa bure katika vituo mbalimbali vya Afya katika utaratibu wa kawaida wa utoaji wa chanjo pamoja na maskuli kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.
“Chanjo hii inatolewa kwa awamu mbili ambapo msichana anapaswa kupata dozi ya kwanza akiwa na umri wa miaka kati ya tisa na 14 na dozi mbili ni miezi sita baada ya dozi ya kwanza.
Alisema lengo la utoaji wa huduma za chanjo ni kuokoa maisha ya watoto kwa maradhi ambayo yamethibitikika kua yanaweza kuzuilika kwa chanjo.
Aliwaomba wazazi,walezi na walimu wa wakuu wa skuli za msingi na Sekondari kuhakikisha kwamba wale wasichana wote wenye umri wa miaka 14 waliopata huduma jumuishi ikiwemo chanjo kuwepo maskulini mwao siku ya Disemba 01 na Disemba 2 kwa ajili ya kupata huduma jumuishi za awamu ya pili.
Sambamba na hayo aliipongeza serikali kufanikisha upatikanaji wa chanjo hiyo kupitia kwa wadau wa maendeleo ya chanjo “immunization partners” ili kukinga kundi kubwa la Wanawake vigori wasiweze kupata saratani ya mlango wa kizazi.