Moja ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar ni kuhakikisha kuwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba wanapata huduma zote bora na muhimu za Afya kwa wakati na kwa haraka.
Katika kufanikisha hilo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekuja na dhana ya OUTSOURCING kwa maana ya kushirikiana na sekta au kampuni binafsi zenye sifa na uwezo wa kutoa baadhi ya huduma zikiwemo za vipimo, usimamizi wa hospitali pamoja na dawa katika hospitali za umma kuanzia ngazi za Wilaya, Mkoa na Rufaa kwa lengo la kupata huduma zenye ubora kwa wananchi wote wanaofika kupata huduma hizo hospitalini na vituo vya afya.
Dhana hii ya kushirikiana na kampuni hizo binafsi imekuja kurahisisha upatikanaji wa huduma zenye ubora kwa wananchi muda wote na kuwezesha kupunguza baadhi ya majukumu kwa Wizara ya Afya.Aidha Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea na majukumu yake ya kusimamia na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapatiwa huduma bora, matibabu mazuri na hapati usumbufu wa aina yoyote anapofika hospitalini.
Kwa kampuni ambazo zimepewa majukumu hayo ni pamoja SAIFEE ambayo ina dhamana ya kusimamia Hospitali za Wilaya pamoja na masuala ya dawa, LANCET ambayo inatoa huduma za maabara, NSK inayotoa huduma za mionzi na ZANZI MEDICAL ambayo ina jukumu la afya za wafanyakazi.
Kampuni zote hizo zinafanya kazi kwa hospitali mpya na kongwe ambapo lengo ni kuhakikisha huduma za afya zinakuwa na ubora wa hali ya juu Zanzibar.