MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema Uwepo wa Mitambo ya uzalishaji wa Hewa Tiba katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Lumumba itaondoa usumbufu wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa katika hospitali zote za Serikali na Binafsi zilizopo hapa nchini.
Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Mitambo ya kuzalisha Hewa Tiba (Oxygen Plants) katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi LUMUMBA,
Amesema hatua ya kufungwa Mitambo hio itarahisisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa na kupunguza gharama ya ununuzi na usafirishaji wa hewa tiba hio amboyo ilikuwa ni kikwazo kikubwa kwa wagonjwa.
Amesema huduma ya HewaTiba itakayozalishwa hospitalini hapo itasambazwa katika hospitali mbali mbali za Serikali na binafsi ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora na ya kisasa na kufikia malengo ya Serikali ya kutoa huduma zilizobora kwa wananchi wote wa Zanzibar kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Taifa.
Amefahamisha kuwa Serikali ya Awamu ya Nane (8) imekuwa ikifanya juhudi kuhakikisha Sekta ya Afya inakuwa na madaktari bingwa na vifaa vya kisasa vya kutolea matibabu bora kwa wananchi jambo ambalo linaakisi Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050 inayolenga kudumisha mfumo wa upatikanaji wa huduma za Afya zenye wataalamu bingwa, teknolojia na vifaa vya kisasa vya utabibu.
Kwa upande wake Waziri wa Afya wa Zanzibar Nassor Ahmed Mazurui amesema kuzinduliwa kwa Mitambo ya Hewa Tiba katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Lumumba kutasaidia kupunguza gharama za ununuzi na usafirishaji wa Oxygen pamoja na kupunguza changamoto ya kukosekana kwa huduma hio.
Amesema upatikanaji wa hewa tiba hio utaamsha ari, kasi na nguvu ya ufanyaji kazi kwa wahudumu wa Afya katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa sambamba na kuwashukuru wafadhili na wasimamizi wote waliosaidia kufanikisha kufungwa kwa mitambo hio wakiwemo wafadhili wakuu Global Fund kwa kutoa ushirikiano uliopelekea kukamilika kwa wakati ufungajibwa mitabo hio na kwa ubora wa hali ya juu.
Aidha ametoa maelekezo kwa wahudumu wa mitambo hio kuitunza na kuifanyia matengenezo kwa wakati uliopangwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma bila ya kusita.
Akitoa taarifa ya kitaalamu Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Amour Suleiman Mohamed amesema mtambo mkubwa unauwezo wakuzalisha oxygen 40 mita cube ambao utaunganishwa na mnyororo wa hewa tiba katika wodi ya kulaza wagonjwa, vyummba vya upasuaji, ICU, kwenye huduma za wagonjwa wa dharura na mtammbo mwengine utazalisha 20 meter cube kwa saa na utatumika kujaza hewa tiba katika mitungi na kusambazwa katika hospitali mbali mbali za Wilaya Unguja na Pemba.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Gobal Fund SARA ASIMWE ameshukuru kwa kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Serikali ya Zanzibar katika kipindi chote cha maadalizi ya ufungaji wa Mitambo hio hadi kufikia hatua ya kuikabidhi Serikalini kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Sara amesema mitambo hio ya hewa Tiba imezingatia ubora na uhitaji wa walengwa ambapo itaweza kutoa huduma kwa Zanzibar nzima kwa kila hospitali itakayokuwa na uhitaji wa tiba hio.
Mitambo hio ya kuzalisha Hewa Tiba imegharimu zaidi ya dola laki nane ambazo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Global Fund ambao ndio wafadhili wakuu wa mradi huo.