Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amewahimiza wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na wizara ya Afya Zanzibar katika kutoa misaada itakayoongeza ufanisi wa utendaji

Wadau na washirika wa maendeleo wamehimizwa kuendelea kushirikiana na wizara ya Afya Zanzibar katika kutoa misaada itakayoongeza ufanisi wa utendaji wa sekta hiyo na kufikia malengo ya serikali ya kutoa huduma za afya za kibingwa kwa jamii.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui wakati akipokea msaada wa dawa kutoka shirika la Global Life Sharing kwa kushirikiana na Taasisi ya Noah ya Nchini Korea Kusini huko Wakala wa Bohari kuu ya dawa Maruhubi.

Amesema Wizara ya Afya ina jukumu la kuhakikisha inalinda afya za wananchi na kuwapatia matibabu mazuri pamoja na kuwakinga maradhi yanayoingia nchini hivyo kuwepo kwa mashirika yanayotoa misaada hiyo muhimu yatasaidia kufikia malengo hayo.

Amesema upatikanaji wa dawa hizo ni muendelezo wa mkataba wa mashirikiano baina ya Wizara ya Afya na Taasisi ya Noah wa kuwapatia misaada ikiwemo mafunzo, dawa pamoja na kuwaunganisha na mashirika ya maendeleo yaliyopo nchini Korea Kusini ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya afya Nchini.

Aidha Waziri Mazrui ameihakikishia taasisi hiyo kuwa dawa zilizotolewa zinafika katika vituo vya afya sambamba na Hospitali zinazohitajika sambamba na kumaliza tatizo lililopo la kukosekana kwa baadhi ya dawa muhimu zinazohitajika na wananchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar Abdulhalim Muhammed Mzale amesema lengo la msaada huo ni kuwafikia wananchi hivyo kwa sasa wanaendelea kuangalia mahitaji ya vituo vya Afya vya Unguja na Pemba kwa lengo la kusambaziwa dawa hizo.

Amesema msaada huo umehusisha dawa zinazohitajika nchini ikiwemo dawa za maumivu, pumu na magonjwa mengine ambayo yanaendelea kusumbua watu wengi hapa Zanzibar.

Mkuu wa Taasisi ya Noah Mama Park sambamba na Mwakilishi wa shirika la Global Life Sharing ya Korea Kusini Mr Kim wamesema matumaini yao ni kwamba msaada huo utahakikisha upatikanaji na vifaa vya matibabu vinavyostahili katika Hospitali na kuimarisha huduma Za Afya zinazotolewa hospitalini humo.

Msaada huo uliotolewa umegharimu dola za Marekani Milioni moja laki Tano sawa na Bilioni Nne nukta mbili kwa fedha za Tanzania.

Loading