Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla azindua kampeni ya chanjo ya polio Mkokotoni

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mkakati muafaka wa kupunguza watu wasio na kinga ili kufikia malengo ya kutokomeza ugonjwa wa Polio Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo katika uzinduzi wa kampeni ya kutoa Chanjo ya matone ya Pilio iliyofanyika katika Viwanja vya Mkokotoni Sokoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya itafanya Zoezi hilo kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ili kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa kuwafikia walengwa waliokusudiwa.

Mhe. Hemed amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika jitihada inazozichukua hasa kwa zoezi hilo na kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo hiyo kwa lengo la kuwakinga na maradhi ya mripuko.

Aidha Mhe. Hemed ameushukuru na kuupongeza  Uongozi wa Wizara ya Afya, Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ pamoja wadau wa maendeleo kwa kusimamia maandalizi ya  zoezi hilo kikamilifu.

Kwa upande wake Waziri ya Afya Mhe. Nassor Ahmed Mazrui ameeleza kuwa miongoni mwa mikakati ya Wizara ni kuhakikisha Zanzibar inasalimika na Maradhi mbali mbali ikiwemo ya Mripuko ambapo juhudi walizochukua ni pamoja na kutoa elimu ya kinga kwa kushirikiana na mashirika ya maendeleo ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la kuhudumia watoto duniani (UNICEF).

Nae Muwakilishi wa Shirika la Afya Duniani anaefanya kazi zake Zanzibar Dr Ande Michael ameeleza kuwa WHO itaendelea kuunga Mkono juhudi za Serikali ikiwemo kupambana na maradhi mbali mbali yakiwemo Polio.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Muhamed Mahmoud ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja imejipanga vyema kusimamia zoezi hilo kwa kuwafikia wananchi wote na kuhakikisha watoto wote wa mkoa  huo wanapata chanjo hiyo.

Loading