RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Hussein Ali Mwinyi, amesema uzinduzi wa boti tano za kusafirishia wagonjwa itaiwezesha serikali kufikia dhamira yake ya kuimarisha sekta ya afya nchini.
Dk. Mwinyi alieleza hayo wakati akizindiua boti Tano za kusafirishia wagonjwa inapojitokeza dharura (Emergency Ambulance Boat) katika uwanja wa Verde Mtoni.
Alisema uzinduzi wa boti hizo ni sehemu ya uimarishaji wa huduma za dharura na mfumo wa rufaa kwa wagonjwa hasa wanaotoka katika visiwa wanaopewa rufaa kutoka vituo vya afya kwenda hospitali za wilaya Mkoa na Taifa.
Aidha alisema lengo la serikali ni kuhakikisha wagonjwa wanafikishwa katika huduma kwa wakati ili kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika ikiwemo vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.
Alibainisha kuwa serikali inatambua kuwa katika visiwa vidogo vidogo kuna changamoto za usafiri wa uhakika wa kusafirisha wagonjwa hasa mama wajawazito wakati wa kujifungua au inapojitokeza dharura yoyote ili kama ajali.
Dk. Mwinyi alisema kutokana na hali hiyo serikali kupitia wizara ya afya imefanya uamuzi wa kutafuta boti hizo maalum kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa ili wananchi wanaoishi kwenye visiwa vidogo vidogo waweze kuondokana na changamoto zinazowakabili wakati wa dharura.
Alitumia nafasi hiyo kuipongeza benki ya dunia kwa kusaidia gharama za ununuzi wa boti hizo na kampuni ya Qiro Limited iliyopewa kazi ya kutengeneza boti hizo ambazo zitatoa huduma za dharura kwa wananchi.
Aliitaka wizara ya afya kuandaa utaratibu mzuri wa kuzisimamia boti hizo ikiwemo kuzifanyia matengenezo kila inapohitajika ili kuhakikisha zinafanya kazi muda wote na kufikia lengo lilokusudiwa.
Hata hivyo, alisema boti hizo zitapelekwa kwenye maeneo yenye changamoto kubwa zaidi na maeneo yaliyobaki yatafanyiwa utaratibu wa haraka baadae.
Aidha alisema ni jambo la faraja na kutia moyo kuona dhamira hiyo ya serikali inaungwa mkono na washirika wa maendeleo ikiwemo mchango mkubwa wa benki ya dunia katika mradi huo.
Aliwasihi wananchi kuendelea kutumia huduma za afya kulingana na taratibu za rufaa zilizowekwa na wizara na kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa dharura yoyote inayojitokeza ili waweze kuwasaidia kupata huduma haraka.
Akimkaribisha Rais Mwinyi, Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazuri, alisema uzinduzi wa boti hizo ambazo zimeshakamilika na tayari kutoa huduma kwa wananchi ni mafanikio ambayo yamekuja kutokana na maelekezo ya Rais Mwinyi kuhakisha kila mwananchi anafikiwa na huduma bora za afya alipo.
Alisema kilio cha wananchi na wahudumu wa afya ni hali mbaya ya usafiri wa dharura katika visiwa vidogovidogo wakati wa dharura na kusabababisha maafa na vifo kwa wananchi lakini ujio wa boti hizo zitasaidia kuondosha changamoto hiyo.
Waziri Mazrui alisema boti hizo zitagaiwa kwenye visiwa vodogo vodogo viliokiwepo Unguja na Pemba ikiwemo Tumbatu, kokota, kojani kisiwa panza.
Alitoa wito kwa watendaji wa afya kuhakikisha hakuna mtu anaekosa huduma hasa kimama kwa kisingizio cha kukosa usafiri wa dharura na badala yake kupambana ili waweze kupunguza madhara kwa wananchi.
Aliipongeza kampuni ya Qiro Group Campany Limited kwa kukabidhi boti tatu na kuamini mbili zilizobaki watakabidhisha ndani ya muda waliokubaliana ndani ya mkataba.
Mbali na hayo, aliipongeza benki ya dunia kwani mbali ya boti tano pia kuna magari 20 ya kubebea wagonjwa, gari la kukusanya damu, magari yakuzolea taka madawa na vifaa tiba zitaingia hivi karibuni.
Mwakilishi wa World Benk DK. Ernest Masaya alisema benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali hasa sekta ya afya kuona wananchi wanapata huduma bora na nzuri. Hivyo, aliahidi kuwa benki hiyo itaendelea kutoa mchango huo kila kunapohitajika.
Dk. Mngereza Mzee Miraji Katibu Mkuu Wizara hiyo alisema boti hizi zimegharimu kiasi cha takriban dola za kimarekani million 100 kwa lengo la kuboresha zaidi huduma za afya nchini na kupatiwa gerentii ya miaka miwili ili
kuhakikisha zinafanya kazi kwa ubora waliokubaliana.
Alisema boti hizo zina kitanda kimoja cha mgonjwa, eneo la wahudumu wa afya wawili, sehemu ya kukaa jamaa wa wagonjwa, vifaa mbalimbali vya kutoa huduma za awali kama Monitor, machine ya kupimia sukari, visaidizi hewa na vifaa vya matumizi ya dharura.
Alibainisha kuwa boti hizo zinatarajiwa kuunganishwa na mfumo wa huduma za dharura zitakazoweza kuonekana kupitia mfumo wa kidigitali ulioko katika kituo cha Afya call center.
Aliwaomba watendaji wenzake kutoa huduma bora na kwa ufanisi ili wananchi waweze kunufaika na huduma hizo.