Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya imefanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Afya kwa kuimarisha huduma zikiwemo vifaa tiba na kuendelea kuwasomesha wafanya kazi ili kuweza kuwa na wataalamu bingwa na ubobezi watakaotoa huduma zenye ubora wa hali ya juu.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla katika ufunguzi wa Mkutano wa majadiliano wa wadau wa maendeleo kuhusu ugharamiaji wa huduma za Afya Zanzibar kwa lengo la kufikia adhma ya Afya bora kwa wote uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar.
Amesema kuwa katika kuhakikisha Serikali inatoa huduma bora za Afya kwa wananchi wote imeamua kufanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya Afya ikiwemo kujenga Hospital kumi(10) kila wilaya pamoja na kuweza kuweka wataalamu bingwa na bingwa bobezi ili kuimarisha huduma bora za afya kwa wananchi wote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ili kuweza kufikia adhma ya Afya kwa wote Serikali imeimarisha hali ya upatikanaji wa dawa nchini, upatikanaji wa chakula kwa wagonjwa sambamba na kuongeza wigo wa utoaji wa matibabu kwa wananchi kama vile huduma ya usafishaji wa figo(DIALYSIS) ambapo kabla wananchi walilazimika kutumia gharama kubwa za matibabu hayo na wengine kupoteza maisha kutokana na kukosa fedha za kugharamia huduma hio.
Makamu amesema kuwa Serikali imeimarisha vifaa vya uchunguzi ikiwemo XRAY, CT-SCAN, MRI, ULTRA SOUND na vifaa mbali mbali vya maabara pamoja na kuimarisha vifaa tiba kwa kujengwa mitambo miwili (2) ya Hewa Tiba (OXYGEN PLANTS) katika hospital ya Mkoa wa Mjini Magharibi – Lumumba ambayo itatumika katika hospital mbali mbali za Zanzibar.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira Bora ya Afya kwa kuajiri wafanyakazi wapya 1,566 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kujenga hospitali za Mkoa, hospital ya Rufaa ya Binguni pamoja na kutoa fursa kwa wafanyakazi wa Afya kujiendeleza kielimi na kuwajengea uwezo madaktari bingwa na binga bobezi kuweza kuleta ilufanisi zaidi katika itoaji huduma za Afya kwa wananchi.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema katika kutatua chamgamoto mbali mbali, Serikali inaendelea kufanya mageuzi katika mfumo wa kugharamia huduma za Afya ikiwemo kuanzisha Mfumo wa Huduma za Afya Zanzibar chini ya Sheria namba 1 ya mwaka 2023 na kupewa jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi wote wanaoishi Zanzibar.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh amesema lengo la kuwepo kwa Mkutano wa ugharamiaji wa huduma za Afya Zanzibar ni kufanya majadiliano ya pamoja kati ya watendaji wa Wizara ya Afya, washirika wa maendeleo na wadau wa Afya ili kupata njia mbadala za kitaalamu ambazo zitaiwezesha Serikali kupitia Wizara ya Afya kuweza kugharamia huduma za matibabu kwa wananchi wote wa zanzibar.
Naibu Waziri amesema gharama za huduma ya matibabu duniani zimekuwa zikipanda siku hadi siku jambo linalopelekea wananchi wengi kutomudu kuchangia huduma hio pale inapobidi hivyo Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imeona ipo haja ya kukaa pamoja na wadau wa maendeelo ili kutafuta namna bora itakayosaidia kupunguza changamoto hio na kuhakikisha kila Mzanzibari anaweza kupata huduma bora za matibabu bila ya malipo yoyote.
Kwa upande wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Mngereza Mzee Miraji amesema katika kipindi hichi cha awamu ya nane Wizara ya Afya imeweza kutekeleza mambo mbali mbali ikiwemo kuimarisha miundo mbinu ya Afya, kuwapeleka watumishi masomoni ndani na nje ya nchi.
Nao washirika wa maendeleo wakiwemo Pharm Access na WHO wamesema kufanyika kwa Mkutano huo utakuwa ni chachu ya upatikanaji wa huduma bora za Afya na zenye usawa kwa wazanzibari wote bila ya malipo.
Wamesema upatikanaji wa huduma bora za Afya unategemea uwepo wa Sera, Mikakati madhubuti, rasilimali watu na rasilimali fedha hasa katika kufikia adhma ya Serikali ya Awamu ya Nane(8) inayolenga kugharamia huduma za matibabu kwa wananchi wake wote.