Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amezitaka Taasisi na Mashirika ya Maendeleo kuimarisha ushirikiano na Taasisi za Elimu ya juu

WAZIRI wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amezitaka taasisi na Mashirika ya maendeleo kuimarisha ushirikiano na taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi pamoja na asasi za kiraia ili kufikia malengo ya Mkakati wa Afya wa Kidijitali wa 2020-2025.

Akifungua mafunzo ya awamu ya Pili ya Afya ya Kidijitali Zanzibar yaliyolenga kujadili na kuchunguza uwezekano wa mabadiliko ya afya ya kidijitali katika kuimarisha afya na ustawi wa jamii Zanzibar yaliyofanyika huko Michenzani Mall.

Waziri Mazrui amesema Zanzibar imejipanga kutumia teknolojia ya kidijitali kuleta mapinduzi katika utoaji wa huduma za afya kwa kuunda mfumo wa afya unaowezeshwa kidijitali ambao ni bora, wenye usawa, na unaomzingatia huduma kwa mgonjwa.

Amesema mpango huo utawawezesha wafanyakazi wa afya ngazi ya jamii (CHWs) kutoa huduma muhimu za afya kwa kuwapa vifaa vya kidijitali vitakavyoimarisha shughuli zao ikiwemo ukusanyaji wa takwimu na zitakazosaidia kuonesha uhalisia wa maradhi yaliyopo kwenye jamii pamoja na miripuko mbalimbali inayotokea nchini.

Amefahamisha kuwa taaluma itakayotolewa kwa wafanyakazi hao ni sehemu ya kufikia malengo ya serikali ya kuhakikisha mifumo ya takwimu na taarifa inakuwa ya kidijitali kwa lengo la kufanya maamuzi sahihi katika kufikia huduma za afya kwa wote na afya bora.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na wananchi washirika wa maendeleo na sekta binafsi, watahakikisha wanadumisha mpango huo ili kufikia vipaumbele vya afya vya kitaifa.

Mbali na hayo ameishukuru taasisi ya D-tree kwa ushirikiano wao katika mipango ya afya ya jamii na uwekezaji wa afya ya kidijitali ambao umesaidia kuongeza ufanisi kwa wahudumu wa Afya ya jamii na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Naibu katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dkt Mzee Suleiman Mndewa amesema kwa sasa miundombinu ya mawasiliano imeimarika hivyo kuja kwa program hiyo kutaendana na kasi ya mawasiliano iliyopo na kuwasaidia kufikia malengo ya watendaji hao.

Ameongeza kuwa ni wakati wa wahaudumu kuongeza ubunifu ili kuhakikisha wanazalisha vitu vingi vitakavyoongeza tija kwenye sekta ya Afya na kufikia malengo ya serikali kupitia wizara ya afya Zanzibar.

Mkurugenzi Kinga na Elimu Ya Afya Dk Salim Slim akawahimiza wahudumu hao kuyatumia vyema mafunzo hayo sambamba na kuwataka kufanya kazi ipasavyo kwa lengo la kupunguza matatizo yaliyopo kwenye jamii ikiwemo sukari, presha pamoja na maradhi yasiyoyakuambukiza.

Mkurugenzi wa D Tree Zanzibar Dr Hannah McCarrick Mikidadi amesema kwa muda mrefu wahudumu hao wamekuwa wakisumbuliwa na matatizo mbalimbali katika utendaji wao hivyo kufunguliwa kwa mafunzo hayo sambamba na kukabidhiwa vitendea kazi vya kidigitali kutasaidia kuifikia jamii kwa haraka pamoja na kukusanya taarifa sahihi jambo litakaloongeza ufanisi wa sekta ya afya nchini.

Msimamizi wa Wahudumua wa Afya ya jamii Bi Halima Ali Khamis amesema kuzinduliwa kwa mfumo huo huo na kukabidhiwa vifaa hivyo vitasaidia katika kupunguza gharama za matibabu kutoa taarifa sahihi za takwimu zinazoongea uwajibikaji kwa CHW, sambamba na kufanya uchunguzi kwa baadhi ya maradhi kwenye jamii.

Jumla ya wahudumu wa Afya ya Jamii 126 wamekabidhiwa simu kwa ajili kuimarisha na utendaji wa kazi zao kidijitali.

Loading