Wizara ya Afya Zanzibar imesaini mkataba wa makubakiano na Shirika la Marekani Electronic Health Network wenye lengo la kuimarisha Sekta ya Afya na kuhakikisha usalama na ubora wa huduma zinazotolewa kuanzia kwenye vituo vya Afya hadi Hospitali kuu.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo huko Vuga Katibu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Mngereza Mzee Miraji amesema Mkataba huo umejikita katika kuboresha rasilimali watu na watendaji wa sekta ya Afya Zanzibar utakaonza kwa kujenga kituo maalumu cha kufundishia watendaji hao.
Ameongeza kuwa mengine yatakayohusika kwenye mkataba huo ni ujengwaji wa miundombinu ya kisasa kuanzia ngazi ya Afya ya msingi hadi hospitali kuu sambamba na uungwanishaji wa mifumo ya ICT jambo litakalotoa wepesi wa upatikanaji wa taarifa kwa ngazi zote.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mkataba huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitano na kufikia malengo ya serikali ya utaoji wa huduma bora na za kibingwa nchini.
Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dkt Amour Suleiman Mohammed amesema mktaba huo utaongeza kasi ya utendaji wa mfuko wa huduma za Afya Zanzibar kwa kupatiwa fedha zitakazotoa nafasi kwa wananchi kunufaika na huduma zinazotolewa na mfuko huo nchini.
Akitoa neno la shukrani Mkurugenzi EHN Jamal Bahabri amesema ni wakati wa taasisi hizo mbili kuongeza ushirikiano hasa pale linapotokea tatizo ili kuchukua hatua zinazofaa kwa kuhusisha pande zote.
Ameongeza kuwa malengo yao ni kuiona Zanzibar inajitangaza kutokana na ubora utakaopatikana katika utoaji wa huduma za Afya jambo litakalotoa fursa kwa nchi nyengine kuja kujifunza nchini .
Mkataba huo umegharimu jumla ya dola za kimarekani Milioni Mia Tatu na Sabiini na Tatu.