Wizara ya Afya Zanzibar kuimarisha Taasisi ya Utafiti wa Afya ZAHRI

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema kuwa inafanya jitihada ya kuimarisha Taasisi ya utafiti wa afya ZAHRI ili iweze kutoa taarifa za kisayansi ambazo zitasaidia udhibiti wa magonjwa wa binaadamu.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi utumishi uendeshaji Mwatoum Ramadhan Mussa katika mkutano wa mashirikiano kati ya Taasisi ya Taifa ya utafiti wa maradhi ya Binaadamu NIMRI na Taasisi ya utafiti wa Afya Zanzibar ZAHRI.

Amesema Katika kuimarisha Taasisi ya utafiti wa Afya hapa nchini Wizara ya Afya itaekeza katika kuajiri wataalamu wenye uwezo wa kufanya tatiti ili kuwezesha kukabiliana na kuondokana na magonjwa mbali mbali.

Amefahamisha kuwa kutokana na mashirikiano yaliyopo baina ya Taasisi ya Taifa ya utafiti wa maradhi ya binaadamu na Taasisi ya utafiti wa Afya Zanzibar kutawezesha kubadilishana uzoefu pamoja na kuwapatia taaluma zaidi watafiti wa Zanzibar kutokana na ujuzi mkubwa walionao.

kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya utafiti wa maradhi ya Binaadamu NIMRI Profesa Said Shebe Aboud amesema lengo la kuja hapa nchini ni utekeletaji wa makubaliano kufuatia kusaini mkataba wa mashirikiano wa kuimarisha masuala mazima ya tafiti.

Amefahamisha kuwa Taasisi ya Taifa ya utafiti wa maradhi NIMRI imepiga hatua kubwa ya utekeletaji wa kazi zao ambapo wana vituo saba kwa Tanzania na Dare es salam ina vituo viwili na wameweza kufanya tafiti mbali mbali.

Amesema wataendeleza ushirikiano na Zanzibar kwa kufanya tafiti, mafunzo kwa wafanyakazi wake kwa kwenda kwenye vituo vyao kikiwemo cha Mbeya ili kuweza kuleta mabadiliko katika Taasisi ya utafiti wa Afya Zanzibar.

Mapema akiwasilisha Ripoti ya Taasisi utafiti wa Afya ZAHRI Mkurugenzi uendeshaji wa ndani katika Taasisi hiyo Bernard Mtuta amesema kuanzishwa Taasisi hiyo kumetokana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutambua umuhimu wa upatikanaji wa taarifa za kisayansi ambazo zitasaidia kupanga mikakati mbali mbali ya tiba na udhibiti wa magonjwa.

Amesema Licha ya Taasisi ya ZAHRI kukabiliwa na uhaba wa wafanyakazi wamewezesha kufanya tafiti mbali mbali kwa kushirikiana na Taasisi nyengine ambapo wameweza kufanya tafiti zikiwemo ya kuangalia hali halisi ya maradhi ya ngozi Micheweni Pemba, utafiti wa miongozo ya jamii kuhusina na uviko 19 pamoja na kupata maoni ya wananchi kuhusina na ugonjwa huo.

Amefahamisha tafiti nyengine waliofanya ni utafiti wa kujua kinga ya maradhi ya uviko 19 katika miili ya Binaadamu pamoja na tafiti ya kwa kina mama waliofikia umri wa kujifungua.

Amesema Taasisi inaendelea na kufanya tafiti mbali mbali ikiwemo ya ongezeko la thamani ya dawa za mitishamba, utafiti wa kujua sababu na viashiria vya ugonjwa wa figo kwa wananchi wa Zanzibar.

Kwa upande wa watafiti kutoka kituo cha utafiti kilichopo Mbeya wameeleza namna ya njia wanazofanya kufikia mafanikio kufanikisha tafiti zao ni kutokana na uwezo ulioimarishwa kutoka Taasisi yao kuu ya NIMRI katika sekta tofauti ikiwemo tafiti zenyewe na masuala ya uchambuzi wa takwimu.

Loading