WIZARA ya Afya Zanzibar imewataka wananchi kuepuka matumizi ya dawa za kienyeji katika kutibu ugonjwa wa macho

WIZARA ya Afya Zanzibar imewataka wananchi kuepuka matumizi ya dawa za kienyeji katika kutibu ugonjwa wa macho ulioikumba jamii katika kipindi cha hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh, alisema, kufanya hivyo kunaweza kuongeza ukubwa wa tatizo hilo na kushauri wagonjwa kufika katika vituo vya afya ili kupata tiba kwa wakati sahihi.

Alisema, ugonjwa huo unaoambukizwa kupitia virusi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwengine, hadi sasa jumla ya wagonjwa 4,579 wameripotiwa katika vituo vya afya na hospitali za serikali na binafsi Unguja na Pemba.

Hivyo, aliwataka wananchi kuchukuwa tahadhari za usafi ikiwemo kunawa mikono marakwa mara katika kujikinga na maradhi hayo.

“Ni muhimu kutambua kwamba hakuna dawa yeyote ya kutibu ugonjwa wamacho unaosababishwa na virusi hawa wa ‘Adenovirus’ matibabu yanalenga kupunguza makali”.

“Maabukizi hutokea mara moja kwa kugusa au kushika maji maji ya mtu aliye na uambukizi wa maradhi haya kama vile matongo, machozi n.k.”.

Alizitaja dalili kubwa za ugonjwa huu wa macho mekundu ni kama jicho kuwa jekundu, kuwasha na kuchomachoma, mifuniko ya macho kuvimba na macho kuogopa mwangaza.

Dalili nyengine ni macho kutoa matongo meupe au ya njano, kuona ukungu kwa uoni wa mbali katika macho,  maumivu ya macho na unaweza ukapata dalili za mafua makali.

Akizungumzia kuhusiana na maradhi yasiyopewa kipaumbele ambapo Zanzibar imeungana na nchi nyengine duniani kuadhimisha siku hiyo,  aliwataka wananchi  kuongeza tahadhari ili kutokomeza maradhi hayo ikiwemo mabusha, matende, kichocho na kipungunya.

Alisema, maradhi yasiopewa kipaumbele (NTDs]) ni maradhi ambayo yanawaathiri zaidi watu masikini kwenye nchi ambazo hazina rasilimali za kutosha.

Alisema, kiujumla, watu wapatao bilioni moja na nusu duaniani kote wanakadiriwa kuwa na maambukizi ya maradhi yasiopewa kipaumbele.

Aliyataja maradhi yasiopewa kipaumbele yanayoisumbua Zanzibar ni kichocho (njia ya mkojo), minyoo ya tumbo na matende. Lakini pia yapo maradhi ya ukoma, vikope, kepu pamoja na upele, na kuumwa na nyoka.

Pia kwa nyakati tafauti kumekuwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa na miripuko ya homa ya dengue.

Alisema, Zanzibar imekuwa ikifuata miongozo na kutekeleza mikakati mbali mbali ya kupambana na kuondoa maradhi yasiopewa kipaumbele ili kuendana na azma na malengo yalio pangwa na Shirika la Afya Ulimwenguni.

Alisema, hivi karibuni tu Zanzibar ilisherehekea kutokomeza ugonjwa wa vikope kama janga la jamii.

Loading