Wizara ya Afya Zanzibar imetangaza rasmi kuwa maradhi ya vikope yameondoka Zanzibar.

WIZARA ya Afya Zanzibar imetangaza rasmi kuwa maradhi ya vikope yameondoka baada ya Shirika la Afya ulimwenguni WHO kuthibitisha kuwa ugonjwa huo sio tishio tena katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui ameyasema hayo katika Mkutano wa kusherehekea na kuipongeza   Zanzibar kuweza kutokomeza maradhi ya vikope kutoka asilimia 11.4 mwaka 2015 na kufikia asilimia 1.2 mwaka 20023 ambapo mkutano huo uliwashirikisha wadau kutoka nchi tofauti pamoja na mashirika ya kimataifa.

Amesema kutokana na jitihada zilizochukuliwa na Serikali yaMapinduzi ya Zanzibar na washirika wa maendeleo wameweza kufanikiwa kuondosha maradhi ya vikope katika Wilaya wa Micheweni Pemba na Kaskazini A Unguja ambapo alibainisha kuwa watahakikisha maradhi hayo hayarajei tena hapa nchini.

Alifahamisha kazi kubwa ilifanyika ya kupambana na maradhi hayo ikiwemo  kulisha dawa, kuwapa matibabu watu ambao walikuwa washaathirika na maradhi hayo pamoja na kutoa elimu sambamba na kufanya tafiti za mara kwa mara kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchi mbali mbali.

Amewataka wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba hasa kwa maeneo ambayo yaliathiriwa na maradhi hayo hapo awali kuhakikisha kuwa wanatekeleza yote waliyopewa na wataalamu sambamba na  kusafisha mazingira yao  ili ugonjwa huo usirejee tena hapa nchini.

Kwa upande wake Mratibu wa huduma za Macho Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Fatma Juma Omar amesema kutokana na jithada zilizofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na washirika wa maendeleo kwa kutoa dawa kwa mzunguko wa mara tatu na ilipofikia mwaka 2021 walifanya utafiti na kubaini kushuka kwa maradhi ya vikope  kuendelea kufanya jitihada Zaidi ya kuondosha maradhi hayo

Amesema kazi iliyopo kwa sasa ni kuzidi kuendelea kuwashajisha wananchi kutekeleza hatua mbali mbali za kujikinga na maradhi hayo ikiwemo kutumia vyoo, matumizi ya maji safi na salama na kuendelea kutoa elimu ya afya kupitia wanafunzi Maskulini na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mpango wa Kimataifa wa kupambana na maradhi ya vikope Dkt Paul Emerson amesema kuwa dunia inajivunia na hatua iliyofikiwa na Zanzibar katika kutokomeza maradhi ya vikope.

Amesema wataendeleza jitihda zilizofanyika na kuhakikisha inakuwa na mashirikiano na mashirika mbali mbali duniani kuona ugonjwa wa vikope unatokomezwa duniani kote.

Loading