WIZARA ya Afya Zanzibar imesema kuwa jitihada kubwa imefanyika ya kumaliza ugonjwa wa vikope katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh amesema jitihada hizo zilizofanywa na Madaktari, wataalamu na washirika wa maendeleo mbali mbali wameweza kufanikiwa kumaliza ugonjwa huo hapa nchini
Akizungumza katika kikao maalum cha kukamilisha ripoti ya kumalizika kwa ugonjwa wa vikope Naibu Waziri amesema ugonjwa huo ambao ulikua katika wilaya ya micheweni mkoa Kaskazini Pemba umeweza kumalizika.
Amefahamisha kuwa kwa zaidi ya miaka kumi Zanzibar imefanikiwa kumaliza ugonjwa wa vikope na kusema kuwa wizara ya Afya Zanzibar pamoja na Tanzania bara kuandaa ripoti maalum na kuiwasilisha katika shirika la afya duniani (WHO) ili kuitangaza rasmi Tanzania bara na visiwani kumalizika kwa ugonjwa huo.
Kwa upande wa Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt Salim Slim amesema Wizara ya Afya itahakikisha inaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya kujikinga na ugonjwa wa vikope na kuwa haurudi tena hapa nchini.
Amesema jitihada kubwa iliyofanywa kukabiliana na ugonjwa huko Micheweni wa kuwafatilia wagonjwa, kutoa elimu na kuhakikisha kuwa hawapati wagonjwa wapya wenye ugonjwa huo na kusema wataendeleza kutoa elimu kwa jamii.
Nae Mratibu wa huduma ya Afya ya Macho Zanzibar Dkt Fatma Omar amesema ugonjwa wa vikope umetokomezwa kwa juhudi mbali mbali ikiwemo ya ulishaji dawa pamoja na ufuatiliaji wa wagonjwa umewezesha kudhibiti ugonjwa huo
Amesema watahakikisha wanatoa elimu kwa jamii katika kujikinga na maradhi ya vikope yasiwe tatizo tena kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Kwa upande wake Meneja miradi maradhi yasiopewakipaumbele Peter Kivumbi amesema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na washirika wa maendeleo tofauti ambao waliunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na ugonjwa wa vikope Tanzania.