Wizara ya Afya itaendeleza mikakati yake kuhakikisha 0 malaria inafikiwa

NAIBU Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh, amesema, wizara hiyo inaendelea na mkakati wake wa kuhakikisha inaendelea kuongoza kufanya vizuri dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa malaria hapa Zanzibar.

Hayo aliyaeleza alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye maadhimisho ya siku ya malaria duniani, hafla iliyofanyika Mnazimmoja.

Alisema, huku taifa likiadhimisha siku hii, hali ya malaria hapa Zanzibar bado ni nzuri ambapo takwimu kwa takriban miaka 10 zinaonesha kuwa tatizo la malaria lipo chini
ya asilimia moja.

Alisema, mafanikio hayo yamepatikana kutokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na serikali ikishirikiana na wadau mbali mbali zikiwemo taasisi za kitaifa na kimataifa za ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, alisema, pamoja na ugonjwa huu kupungua, bado ugonjwa wa malaria upo Zanzibar huku takwimu za mwaka 2022 zikionesha wagonjwa 4, 557 walioripotiwa na kuthibitishwa kuwa na ugonjwa wa malaria ukilinganisha wagonjwa 6,096 walioripotiwa mwaka 2021.

Alisema, takwimu hizo zilionesha kupungua kwa wagonjwa wa malaria kwa asilimia
42.2, hivyo ipo haja ya kuendelea kuchukuwa tahadhari kwa kuweka mazingira safi ili kuepuka mazalio ya mbu wanaosababisha malaria.

Aidha, alisema, pamoja na mafanikio hayo makubwa, bado kuna changamoto zinazozuia kumaliza kabisa malaria Zanzibar, ikiwemo ushiriki mdogo wa taasisi mbali mbali  katika mapambano hayo.

“Ugonjwa wa malaria kwa wasafiri wa ndani (Unguja/Dar es Salaam, Tanga,
mikoani Tanzania Bara bado ni changamoto inayohitaji msaada mkubwa
kutoka serikali za mikoa na wilaya”alisema.

Alisema, takwimu zinaonyesha kuwa kati ya wagonjwa 4,557 walioripotiwa mwaka
2022, wagonjwa 3, 938 sawa na asilimia 80 walikua na historia ya kusafiri nje ya
Zanzibar kutoka katika maeneo tofauti ya Tanzania Bara.

Kaimu Meneja Mradi wa Kumaliza Malaria Zanzibar, Dk. Shija Joseph, alisema, asilimia 80 ya wagonjwa wanaogundulika na malaria wamekuwa wakitoka nje ya Zanzibar hivyo wameandaa mkakati wa kuwapima na kuwatibu kwa kuwafuatilia katika maeneo wanayoishi.

Siku ya Malaria Duniani huadhimishwa kila ifikapo Aprili 25 ambapo kauli mbiu mwaka huu ni  ‘Ushirikishwaji wa Taasisi na Jamii ni Kipaumbele cha Kumaliza Malaria Zanzibar.’

Loading