WAZIRI wa Afya Zanzibar amesema mapambano ya kumaliza maradhi yasioambukiza Zanzibar yanahitaji nguvu ya pamoja

WAZIRI wa Afya Zanzibar Nassro Ahmed Mazrui amesema mapambano ya kumaliza maradhi yasioambukiza Zanzibar yanahitaji nguvu ya pamoja na wadau ili kuwa na taifa salama lisilo na maradhi.

Amebainisha hayo katika mkutano wa wadau ulokuwa na lengo la kujadili mbinu za kumaliza maradhi yasiyoambukiza

Amesema mabadiliko ya mtindo wa maisha ndio chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kutokufanya mazoezi ya kutosha na tabia bwete ambyo husababisha kuongezeka kwa uzito wa mwili 

Meneja Mradi kutoka Pharm Access Dkt Faiza Abasi amesema kuwa maradhi yasiyoambukiza yameathiri watu wengi hapa Zanzibar hali inayopelekea kupoteza nguvu kazi ya jamii.

Dkt Faiza amesema kuwa ni wajibu wa kila mwanajamii anatakiwa kuja na mbinu za kukabiliana na maradhi yasiyoambukiza na sio kuiachia serikali peke yake katika mapambano haya.

Kwa upande wake Afisa kutoka Kitengo cha maradhi yasiyoambukiza Dkt Lulu Omar Bakar amesema zaidi ya watu elfu tatu wanasumbuliwa na maradhi yasiyoambukiza Zanzibar kwa mujibu wa takwimu za Kitengo cha maradhi yasiyoambukiza Zanzibar

Dkt Lulu amewataka watu wanaoishi na maradhi yasiyoambukiza kuacha tabia ya matumizi ya tiba za dawa za asili ambazo hazijathibitishwa kitaalam ili kujiepusha na madhara ya dawa hizo

Akiwasilisha mada juu ya maradhi yasioambukiza Mwenyekiti NCD alliance tanzania Prof.Andrew Swai amesema kuwa ili tukabiliane na maradhi yasiyoambukiza ni wajibu wa kila mtu kuacha tabia ya kula vyakula vya nafaka vilivyokobolewa pamoja na ukamuaji wa matunda

Kwa mujibu wa Shirika la Afya ulimwenguni WHO maradhi yanasababisha vifo vingi zaidi duniani ni ugonjwa wa moyo ambapo watu milioni 17.9 kila mwaka hufariki kutokana na ugonjwa huo, huku ukifatiwa na saratani watu milioni 9.3 hufariki kila mwaka, ugonjwa wa kisukari ukichukua nafasiya tatu watu milioni 2.0 hufariki kila mwaka.

Loading