Wanafunzi wa Skuli ya Maandalizi Kidutani wamepatiwa huduma za Upimaji wa Afya na madaktari kutoka China

JUMLA ya watoto 400 wa Skuli ya Maandalizi ya Kidutani wamepatiwa huduma ya upimaji wa afya ili kuhakikisha wanakuwa na afya njema.

Zoezi hilo lililofanyika skuli hapo, liliendeshwa na timu ya Madakari wa Kujitolea kutoka China ambapo watoto hao walipatiwa uchunguzi tofauti ikiwemo upimaji wa macho, masikio, vinywa na shinikizo la damu.

Akizungumza kwenye zoezi hilo, Mkuu wa Madakari kutoka China, Profesa Jiang Guoqing, alisema, lengo la upimaji afya huo ni katika jitihada za kuwasaidia watoto kwa ajili ya kutambua afya zao na kupatiwa matibabu watakapogundulika na matatizo.

“Leo tumekuja kufanya uchunguzi wa kiafya kwa watoto kwa kutambua umuhimu mkubwa kwa ajili ya makuzi yao ya baadaye”.

“Watoto ndiyo ndiyo taifa la baadaye, huduma za kiafya ni jambo la msingi kwao”.

Aidha, aliishukuru Wizara ya Afya na Serikali kwa namna zinavyotoa ushirikiano mkubwa madaktari wa Kichina wanapofika Zanzibar kwa ajili ya kutoa huduma mbali mbali.

Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Maandalizi Kidutani, Asma Ali Yussuf, zoezi hilo litawasaidia kutambua afya za watoto hao na kuwaweka salama katika kuwajengea mustakabali bora wa masomo yao.

“Sisi kama uongozi wa Skuli tumeupokea msaada huu kwa mikono miwili, tukiamini afya njema za watoto ndiyo tumaini la taifa”.

Alisema, wamekuwa na utaratibu wa kuwapima watoto afya kwa kila kipindi na kwamba msaada huo wa timu ya Madaktari wa Kichina utaendelea kuwa chachu kwao kwa ajili ya maendeleo ya watoto hao.

Nao baadhi ya wazee wa watoto hao walielezea kufurahia kutolewa huduma hiyo na kuiomba serikali na wizara ya afya kuendelea kufanya zoezi hilo kila mara ili kuwaweka watoto kwenye afya njema.

Loading