Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya Zanzibar imempokea Princess Sophie (Duches of Edinburgh) kutoka Uingereza ambae yupo nchini kwa ziara ya siku mbili.
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema lengo la kufika hapa nchini ni kuangalia maendeleo ya miradi ya sekta ya Afya inayofadhiliwa na nchi hiyo inayotekelezwa katika maeneo mbali mbali.
Akimpokea Mgeni huyo huko katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Waziri Mazrui amesema lengo la kuja kwake ni kuangalia utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na inavyowafikia walengwa.
Amesema ni miaka kumi na mbili sasa nchi ya Uingereza imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika maradhi yasiyopewa kipaumbele ikiwemo dawa za Matende, Kichocho maradhi ya macho na mabusha, dawa za safura na maradhi mengine mbali mbali ili kutokomeza maradhi hayo.
Ameongeza kuwa ziara hiyo itasaidia kuongeza ushirikiano wa misaada mbali mbali ikiwemo ya dawa na matibabu baina ya nchi hizi mbili jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi na kumaliza maradhi ambayo yamekuwa yakiwasumbua watu mbalimbali nchini.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amesema mkoa wake ni moja miongoni mwa maeneo yaliyonufaika na misaada hiyo ikiwemo maeneo ya Masumbani Kinuni na maeneo mengine ili kujionea hali halisi za wanufaika wa misaada yao waliyokuwa wakiitoa kwa Zanzibar.
Aidha amempongeza Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Dk Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zao wanazozifanya katika kuhakikisha Tanzania zinapata washirika mbalimbali wanayounga mkono utekelezaji wa miradi yake.
Aidha amewataka wananchi wa mkoa wa mjini magharibi kutoa ushirikiano kwa mgeni huyo kwa siku zote atakazokuwepo nchini ili aweze kujionea ukarimu na uzuri wa utamaduni Zanzibar