Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Serikali ya Switzerland

 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Serikali ya Switzerland katika kuongeza juhudi za kumaliza malaria nchini.

Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui aliyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Ubalozi wa Switzerland nchini Tanzania ofisini kwake Vuga.

Alisema Serikali ya Switzerland inashirikiana na Tanznaia katika kumaliza malaria kwa kusaidia katika kutoa mfaunzo, vifaa pamoja na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kitengo cha malaria.

Aaidha amefahamisha kuwa Switzerland imesaidia kuanzisha mfuko wa Bima ya afya Zanzibar kwa kutoa nyenzo na mafunzo hadi kuzinduliwa kwake, hivyo uwepo wake unaendelea kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kumaliza malaria nchini pamoja huduma za Afya ya mama na mtoto.

Aliongeza kuwa Switzerland kwa kushirikiana na UNFPA wameendelea kutoa mchango wao katika masuala ya uzazi wa mpango na afya ya mama na mtoto na malaria kwa lengo la kuifanya Tanzania iendelee kuimarika na kutoa huduma bora katika maeneo hayo.

Tumewasifu sana kwa mashirikiano yao na misaada yao wanayotupa na tunaomba wandelee kutusaidia pamoja na kuendelea kuwapatia mafunzo watendaji wetu” aliongeza Waziri Mazrui.

Kwa upande wake Mkuu wa mashirikiano ya Kimataifa katika ubalozi wa Switzerland nchini Tanzania Holger Tausch alimuhakikishia Waziri Mazrui kuwa wataendeleza mashirikiano yao yaliopo ambayo yametimiza mika 60 sasa katika sekta ya Afya na inaendelea kuimarika hasa kwa kusaidia kwenye upande wa mafunzo pamoja na baadhi ya maeneno muhimu watakayokubaliana.

Sambamba na hayo alisisitiza kuwa wataendelea kuandaa mpango wa kumaliza malaria unayafikia maeneo yote ambayo bado imekuwa tatizo kuyafikia kutokana na uhaba wa nyenzo na matatizo mengine mbalimbali.

Kwa upande wa Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt Salim Slim amesema Wizara ya Afya inaendelea kuchukua hatua mbali mbali za kupambana na Malaria ili isiweze kuathiri wananchi wa Zanzibar na amesifu jitihada za Switzerland za kusaidia kuunga mkono jitihada za Serikali.

Ushirikiano baina ya Switzerland na Tanzania umefikia muda wa miaka sitini (60) sasa.

 

Loading