Rais wa Zanzibar amefungua jengo la Huduma za Tiba za Dharura na Maabara katika kituo cha Afya Makunduchi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema Ujenzi wa jengo jipya la huduma za matibabu ya dharura na maabara ya kisasa ni miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha miundombinu ya huduma za Afya ili ziweze kwenda sambamba na mabadiliko ya maendeleo ya huduma za afya duniani.

Akizungumza mara baada ya kufungua jengo la huduma zaTiba  za dharura na Maabara katika kituo cha Afya Makunduchi Dkt Mwinyi amesema Amesema kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua mbali mbali za kuimarisha huduma za Afya katika ngazi zote ili wananchi waweze kupata huduma  kwa ukaribu na zenye ubora.

Amesema Hatua hiyo ni ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020- 2025 pamoja na ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Aidha alifahamisha kuwa  Katika sekta  ya afya utekelezaji  umefanyika  kwa kumaliza kujenga na kufungua hospitali 10 za wilaya na moja ya Mkoa ya Lumumba ambazo zote zimewekwa  vifaa vya kisasa na wataalamu kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi kwa mujibu wa ngazi ya hospitali husika.

Amesema Serikali ya  Awamu ya Nane itaendelea  kujenga hospitali za mikoa katika mikoa iliyobaki ikiwemo Mkoa wa Kusini Unguja ambapo tayari  mfadhili ameshapatikana na  Eneo lipo tayari na mfadhili ameshawasilisha michoro ya awali ya hospitali hiyo itakavyokuwa.

Alisema Kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itaendelea  kuimarisha upatikanaji wa huduma za Afya kwa ngazi ya msingi ambapo Hatua hiyo ni utekelezaji wa mpango mpya wa serikali katika utoaji wa huduma za Afya ngazi ya msingi ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu kwa kujenga majengo mapya na kutanua  baadhi ya vituo vya afya nchi nzima.

Ujenzi huo utaenda sambamba na kuweka vifaa vya kisasa kwa lengo la kutoa huduma bora za afya ikiwemo za dharura na uchunguzi wa awali katika ngazi ya msingi kwa lengo la  kupunguza vifo visivyotarajiwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Hassan Khams Hafidh amesema sekta ya afya imeweza kupiga hatua kubwa kwa awamu hii ya nane ambapo hospitali zimejengwa na kuwekwa vifaa vya kisasa na kuongezeka kwa vitanda vya kulaza wagonjwa pamoja huduma za wagonjwa zimeimarika.

Amewataka wahudumu wa afya  kutoa huduma zenye ubora kwa wananchi wanaofika kupata huduma mahospitalini ili kuweza kuondokana na malalamiko kwa wananchi.

Kwa upande wa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt Amour Suleiman Mohamed amesema  kituo hicho cha afya kilikuwa kinatumika kama hospitali ya Wilaya na ilikuwa inatoa huduma kwa zaidi ya wananchi 63,156 wa shehia zote za 21 za Wilaya ya Kusini.

Hospitali hiyo ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya kutokuwepo kwa jengo la matibabu ya dharura na maabara kulikuwa na  chumba kimoja tu ambacho hakiendani na ubora wa huduma za maabara kwa mujibu wa miongozo iliyopo.

Aidha amefahamisha kuwa  ufadhili wa jengo hilo washirika wa maendeleo HIPZ kupitia Lady Fatemah trust na Action Medeor pamoja na kusimamia ubora wa huduma zitolewazo kituoni hapo ambapo limegharimu shilingi  650 milioni, vifaa tiba vyenye thamani ya milioni 150.

Kwa upande wa wafadhili waliosaidia kujenga jengo hilo Mukhtar Karim kupitia lady Fatemah Trust amesema lengo la kujenga ni kuimarisha huduma za afya zikiwemo ya mama na mtoto ili kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuimarisha huduma za afya ya akili hapa nchini.

Amesema wataendelea kusaidia sekta ya afya hapa nchini katika Nyanja tofauti  ikiwemo mama na mtoto, afya ya akili, vifaa pamoja na utaalamu kwa wafanyakazi wake

Kwa upande wake mwakilishi kutoka HIPZ Simon Kuhnet amesema wataendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapunduzi ya Zanzibar katika kuimarisha huduma za kijamii.

Amesema HIPZ imeweza kutekeleza kazi zake hapa nchini kwa kuimarisha mindo mbinu ya afya, vifaa tiba pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa sekta ya afya.

Loading